Dondoo

Afuta harusi kugundua baba mkwe ni mganga

August 4th, 2019 1 min read

NA JOHN MUSYOKI

KIRITIRI, EMBU

JAMAA wa hapa alikatiza mpango wa kuoa kwa harusi alipogundua kwamba baba ya demu aliyekuwa akichumbia alikuwa mganga.

Penyenye zinasema jamaa hakuwa ameenda kuwaona wazazi wa demu. Juzi, aliandamana na demu hadi kwao kupata baraka za wazazi na akapigwa na butwaa kupata baba ya demu akiendelea kuwahudumia wateja wake.

Inasemekana baada ya mazungumzo na mzee huyo, jamaa aliondoka akiwa na mawazo kwa sababu hakutarajia kuwa baba ya mpenzi wake alikuwa mganga.

Jamaa aliporejea kwao alishangaza watu kwa kutangaza kwamba hangeendelea na mipango ya harusi. “Samahani, arusi haitafanyika kama ilivyopangwa. Kuna jambo ambalo ningependa kulitatua kabla ya arusi kufanyika,” jamaa aliwaambia wazazi na marafiku wake.

Wazazi wa jamaa walipigwa na mshangao na kutaka kujua ni kwa nini mwanao hakutaka arusi ifanyike.

“Tumejiandaa kwa muda mrefu. Ni kwa nini umeanza kuharibu mambo. Umepata msichana mrembo wa kuoa, kulikoni?” mama yake alimuuliza.

Inasemekana jamaa alifunguka na kuelezea sababu ya kufutilia mbali arusi yake. “Juzi nilipotembelea wazazi wa demu nilipigwa na mshangao nilipogundua baba yake ni mganga. Kwa sasa nahofia kuoa msichana wake kwa sababu huenda nikaandamwa na nuksi,” jamaa alisema.

Watu kijijini walishangazwa na uamuzi wa jamaa huyo. Inasemekana wazazi na majirani wa jamaa huyo walimshawishi aoe demu huyo lakini jamaa alikataa katakata.

“Sitamuoa kwa sababu hakunifahamisha mwenyewe kwamba baba yake ni mganga. Hii inaonyesha sio wa kuaminika,” jamaa alisema

Hata hivyo, haikujulikana kilichojiri baada ya kioja hicho.