Makala

AFYA: Cha kufanya ili kupata usingizi wa kutosha

June 12th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

USINGIZI wa kutosha ni muhimu kwa ajili ya afya ya mwili wako.

Hata hivyo, kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, pamoja na kujengeka kwa jamii yenye mfumo wa maisha yenye shughuli nyingi, watu wengi hawapati usingizi mzuri.

Ni muhimu kujaribu kutafuta muda ili kulala vizuri. Baadhi ya manufaa ya kulala au usingizi mzuri ni kama vile;

 • Huimarisha na kuboresha ukuaji wa mwili.
 • Hujenga na kuimarisha kinga-mwili.
 • Hukuweka katika hali nzuri (mood).
 • Hukuongezea kumbukumbu.
 • Huondoa msongo wa mawazo.

Huu utaratibu ni muhimu:

Punguza mwanga wa rangi ya bluu jioni na usiku

Mwanga huu hupatikana hasa katika vifaa vya kielektroniki kama simu, kompyuta na hata runinga. Utafiti unaonyesha kuwa mwanga huu wa bluu hupunguza uzalishaji wa homoni ya “melatonin” ambayo ndiyo hutupa usingizi.

Inashauriwa kuepuka kutumia mitandao ya kijamii au kutazama vitu katika vifaa vilivyotajwa hapo juu usiku ili kuboresha usingizi wako. Vifaa hivi visikufanye kuwa mtumwa.

Kaa palipo na mwanga wa kutosha mchana

Unapokaa kwenye mwanga wa kutosha mwili wako utaweza kutambua ni wakati upi umeamka na ni wakati gani wa kulala. Mwili utafanya mazoea ya kubaini kuwa sasa ni usiku na ni wakati wa kulala kwani mchana kutwa hukuwa umelala.

Epuka matumizi holela ya caffeine jioni au usiku

Sokoni leo vipo vinywaji kadha vilivyotengenezwa au kuongezewa caffeine.

Matumizi ya caffeine huamsha na kuchangamsha mwili wako na kuuweka katika hali ya kutojipumzisha.

Hivyo, matumizi ya caffeine jioni au usiku yatasababisha mtu kutopata usingizi mzuri. Vinywaji vyenye caffeine nyingi ni kama vile kahawa pamoja na baadhi ya soda na vinywaji vya kuupa mwili nguvu maarufu energy drinks.

Punguza au acha kulala mchana

Mara ngingi unapolala mchana ni sawa na kusema umepunguza usingizi wa usiku. Ni vyema ukajitahidi kutolala ili kukupa usingizi wa kutosha wakati wa usiku.

Zingatia ratiba ya kulala na kuamka

Ukiwa umelala kwa zaidi ya muda uliozoea, ukiamka si ajabu ujihisi umechoka ajabu!

Vivyo hivyo, kwa siku uliyochelewa kulala pia.

Hivyo basi, jitahidi kulala na kuamka kwa wakati unaofanana ili mwili wako uweze kufuata utaratibu ambao umeuzoea.

Boresha mazingira ya chumbani unamolala

Hakikisha unalala katika chumba ambacho hakina mwanga mwingi, joto kali, baridi, uhaba wa hewa safi au kelele.

Cha kufanya ili kuboresha chumba chako:

 • Zima au punguza mwanga katika chumba chako.
 • Zima redio, televisheni au kifaa kingine kinachosababisha kelele.
 • Fungua madirisha ili kuhakikisha unapata hewa ya kutosha.

Usile sana usiku au usile vyakula vizito usiku.

Kutokana na watu wengi kuwa na shughuli nyingi wakati wa mchana, hushindwa kula vyema mchana hivyo wanapendelea kula sana usiku.

Hili si jambo zuri kwani mwili unakuwa umepumzika wakati wa usiku. hivyo kula sana kutapelekea mwili kutumia nguvu nyingi kumeng’enya chakula hicho. Ndiyo maana watu wengi wanaopendelea kula sana usiku huamka asubuhi wakiwa wamechoka sana au wamefura tumbo.

Pumzisha akili yako jioni

Kuna umuhimu wa kusoma au kusikiliza vitu vyenye kuburudisha na kuliwaza akili yako jioni kwani kutafanya akili yako kukuruhusu kupata usingizi wa uhakika. Cha kufanya:

 • Epuka kutazama au kusikiliza filamu au masimulizi ya kutisha.
 • Sikiliza redio kwa sauti ndogo jioni.
 • Soma vitabu vyenye maandiko ya kuliwaza na kuburudisha.

Oga jioni au kabla ya kulala

Kuoga jioni au usiku kabla ya kulala kutauweka mwili wako katika hali nzuri kiafya na kukufanya kulala vyema. Hivyo unaweza kuoga kabla ya kulala ua hata kusafisha miguu yako kwa maji kabla ya kulala ili kukuwezesha kupata usingizi mzuri.