Makala

AFYA: Faida za kufunga kula (fasting)

June 11th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WATU wengi wanafahamu kuwa kufunga kula ni suala linalohusiana na imani za kidini. Wengi hawafahamu kuwa kufunga kula kuna manufaa ya kiafya pia.

Kufunga kula ni tendo lenye historia ndefu sana.

Huboresha metaboli

Metaboli ni mchakato ambao mwili hutumia virutubisho kutoka kwenye vyakula ili kujipa nguvu.

Unapofunga kwanza unapumzisha mfumo wako wa umeng’enyaji. Pili, unaufanya mchakato wa metaboli kwenda vizuri kwani mwili utatumia vyema virutubisho vilivyoko mwilini tayari.

Huboresha mzunguko wa damu

Kufunga kula hufanya mzunguko wa damu uende vizuri hasa kwa watu wenye aina ya pili ya ugonjwa wa kisukari (Type 2 Diabetes). Hata hivyo, auguaye kisukari anashauriwa kupata ushauri wa daktari kufahamu kama kweli anaruhusiwa kufunga au la. Si vizuri mtu kujilazimisha matokeo yakawa ni kujidhoofisha kabisa kiafya.

Husaidia kupunguza uzani

Kufunga kula ni njia mojawapo iliyo bora zaidi kupunguza uzani kwani kwa njia hii, mwili hutumia mafuta yaliyoko mwilini ili kujipa nguvu.

Hufanya insulini kufanya kazi vizuri

Unapofunga kula mwili huzalisha insulini ili kudhibiti kiwango cha sukari mwilini kwani hakuna sukari inayoingia. Kwa njia hii insulini itaweza kuzalishwa na kufanya kazi ipasavyo mwilini mwako.

Hupunguza shinikizo la damu

Watu wengi wanapofunga hujikuta pia shinikizo la damu likipungua, hii inasababishwa na kupungua kwa kiwango cha chumvi kwenye damu.

chumvi nyingi husababisha shinikizo la damu. Hivyo kufunga ni kupunguza kiasi cha chumvi kinachoingia mwilini.

Husaidia kutawala sukari mwilini

Kwa watu wenye kiwango kikubwa cha sukari mwilini, wanaweza wakatumia njia ya kufunga ili kuipunguza. Kumbuka unapofunga unapunguza pia kiwango cha sukari kinachoingia mwilini.

Huboresha utendaji kazi wa ubongo

Kufunga kula kunachochea uzalishaji wa protini ya brain-derived neurotrophic factor (BDNF) ambayo ni muhimu sana katika ukuaji, afya na utendaji kazi wa seli za fahamu za ubongo (neurons).

Huboresha afya na mwonekano wa ngozi

Ingawa lishe bora ni muhimu kwa ajili ya afya ya ngozi, kufunga kula kunaifanya ngozi iwe na mwonekano mzuri.

Ngozi inapokuwa na sukari nyingi, huifanya iwe na mwonekano usiovutia.

Kwa kufunga kula utapunguza kiwango cha sukari kinachoingia mwilini, hivyo kuwa na ngozi yenye mwonekano mzuri.

Huwezesha kujizalisha upya kwa seli

Seli hukua na kuchakaa au hata kufa kwenye mwili wa binadamu. Kama ilivyo kwa kinga mwili, utafiti unaonyesha kuwa unapofunga, mwili huzalisha seli mpya ili kujiandaa au kukabili badiliko lolote linaloweza kutokea.

Husaidia kutawala umbo la mwili na mwonekano

Njia nzuri ya kutawala umbo au mwonekano wako ni kwa kutawala kile unachokula. Hii ndiyo sababu walimbwende au warembo hujizuia sana kula ovyo ili wasije wakaharibu mwonekano wao.

Kwa kuhitimisha, ni dhahiri njia ya kufunga kula itamsaidia mtu kutawala umbo na mwonekano wa mwili; ikiwa unataka uwe ama mnene au mwembamba.