Makala

AFYA: Faida za mabamia

May 14th, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

BAMIA ni tunda refu lililochongoka lenye mbegu ndogondogo ndani yake ambalo hupikwa na kutumiwa kama mboga nzuri inayohusishwa pakubwa na kutibu magonjwa mbalimbali katika ngozi ikiwa pamoja na kufanya ngozi ya mlaji kuwa nyororo kutokana na uteute uliomo katika bamia ambao husaidia kuunda tishu za mwili na ngozi.

Lakini pia bamia huusika kutibu chunusi ambazo huwa ni kero kwa watu wengi.

Cha kufanya na bamia ili kutibu chunusi

Unahitaji:

  • mabamia matano
  • limau moja na maji kidogo

Chukua mabamia yako uyakatekate na uyasage kwenye chombo chako cha kusagia kama vile blenda au kinu.

Chukua kipande cha limau na maganda yake na pamoja na maji kidogo, saga kwa pamoja.

Baada ya kupata mchanganyiko huo, paka usoni hadi kwenye shingo.

Acha kwa muda kisha osha.

Inashauriwa kufanya kitendo hiki kwa muda wa siku tatu kwa wiki.

Mbali na kufanya hivyo, mtu anashauriwa kula mabamia kwa wingi kwani yana wingi wa vitamini A ambayo husaidia kutengeneza kinga dhidi ya sumu (toxins). Hii ina maana kwamba sumu inapoingia mwilini, bamia huzuia kusambaa kwake.

Vitamini A husaidia kuupa mwili kinga ya kupigana na maradhi yatokanayo na virusi lakini pia kwa wale wenye matatizo ya kuona, mabamia husaidia kuimarisha mwanga katika macho.

Wingi wa vitamini A huzuia maradhi yatokanayo na virusi kama vile mafua.

Kwa kuhitimisha pia ni muhimu kujua kwamba mabamia yamesheheni Vitamini K ambayo husaidia kuimarisha mifupa na kuganda kwa damu kuzuia umwagikaji mwingi wa damu mtu apatapo jeraha.