Makala

AFYA JAMII: Kidume cha mbegu au goigoi chumbani?

October 22nd, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

KUKOSA mtoto ni miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha ndoa kuvunjika na mara nyingi wanaume hukimbilia kuwalaumu wake zao.

Lakini ukweli ni kwamba wanaume huchangia kwa kati ya asilimia 40 na 50 kwa wanandoa kushindwa kupata mtoto.

Hii ni kutokana na mwanaume kuwa na mbegu haba au dhaifu zisizoweza kutungisha mimba.

Kwa kawaida mwanaume anaposhiriki tendo la ndoa anafaa kuachilia kati ya mbegu milioni 40 na milioni 200 kwa kila ‘safari’.

Lakini mwanaume anapotoa chini ya mbegu milioni 40, kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kutungisha mimba, kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO)

Kwa kutojua hili, wanaume wengi wanapokosa watoto, huanza kuwalimbikizia lawama wake zao na hata kuamua kuoa wanawake wengine.

Mwanaume anaweza kujuaje kwamba ana mbegu chache au hafifu?

Kwa kwenda hospitalini, watapimwa na kutibiwa na wanaweza kupata watoto.

Watafiti pia wamegundua kifaa kinachowezesha wanaume kutumia simu zao kujipima na kufahamu ikiwa mbegu zao za kiume zina uwezo wa kutungisha mimba au la.

Kwa kutumia kifaa cha YO Home Sperm Test, wanaume pia wataweza kulinganisha mbegu zao na zile za wanaume wengine kote duniani.

Kifaa hicho kimeunganishwa na takwimu za WHO ambapo mwanaume anapata fursa ya kulinganisha ubora wa mbegu zake na za wanaume wengine.

Kilitengenezwa na kampuni Medical Electronic Systems, iliyoko Los Angeles, Amerika.

Kampuni hiyo inadai kuwa kifaa hicho kitasaidia wanaume kuepuka aibu ya kwenda kwa daktari ili kufahamu hali ya mbegu zao za kiume.

Aidha kiliidhinishwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Vyakula na Dawa nchini Amerika (FDA) miaka mitatu iliyopita.

Teknolojia hiyo inayodaiwa kutoa matokeo sahihi kwa asilimia 97, huorodhesha ubora wa mbegu za kiume kwa kuzipatia alama ya kati ya 0 na 100.

Mbegu zinazopewa alama ya chini ya 40 zinamaanisha kwamba hazina uwezo wa kutungisha mimba.

Mbali na kifaa cha YO, watafiti katika Chuo Kikuu cha Matibabu cha Harvard, Amerika pia wanaendelea na harakati za kutengeneza teknolojia nyingine ambayo itasaidia wanaume kupima mbegu zao za kiume kwa kutumia simu.

Kupitia teknolojia hiyo, kamera ya simu ndio itatumika kama darubini ya kupima mbegu.