Makala

AFYA: Kitunguu saumu kina faida zozote kiafya?

April 3rd, 2019 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KITUNGUU saumu ni jamii ya vitunguu na htumika kama kiungo katika mboga na vilevile katika tiba na afya.

Kitunguu saumu kinatibu maradhi mbalimbali yanayosababishwa na bakteria, matatizo katika mapafu na matatizo katika mfumo wa umen’genyaji chakula.

Kinaweza pia kutumika kama dawa ya kusafishia vidonda na kuzuia kidonda ndugu. Zipo dawa kadhaa zilizotengenezwa kwa kutumia jamii hii ya vitunguu saumu ikiwemo dawa ya kusafisha mdomo (mouth wash).

Faida za vitunguu saumu

Vina uwezo wa kutibu maambukizi ya bakteria, fangasi na virusi vya aina mbalimbali.

Pia husaidia kuzuia magonjwa ya moyo kwa kusaidia katika kurekebisha shinikizo la damu.

Vitunguu saumu husaidia kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Hata hivyo, inashauriwa kwamba wagonjwa wa kisukari wanaotumia sindano za insulin wasitumie kitunguu saumu kwa wingi mpaka watakaposhauriwa na daktari.

Ina kiasi kikubwa cha vitamini C

Ukiacha faida zake, vitunguu saumu pia vina hasara na madhara mbalimbali kwa mtumiaji. Baadhi ya athari hasi ni pamoja na kuchangia harufu mbaya kuhanikiza kinywani. Hata hivyo, madhara haya yanaweza kupunguzwa kwa kunywa maziwa au kunywa maji mengi.

Kwa baadhi ya watumiaji, vinaweza kuwaletea mzio au mcharuko mwili (allergies au inflammatory reactions).