Makala

AFYA: Kucheza na sabuni kwaweza kumletea mtoto asthma

February 25th, 2020 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

Unahifadhi wapi sabuni baada ya kufua nguo, kuoga au kuosha vyombo nyumbani? Ikiwa unaweka katika sehemu ambayo inaweza kufikiwa na watoto, basi umekuwa ukiwaweka hatarini kupatwa na maradhi ya pumu (asthma) bila kujua.

Watafiti sasa wanasema kuwa watoto wachanga wanaochezea sabuni mara kwa mara wako katika hatari ya kupatwa na maradhi ya asthma.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Simon Fraser cha nchini Canada ulihusisha watoto 2,000 wa umri wa chini ya miezi minne.

Watoto hao hawakuwa wamewahi kuwekwa katika mazingira yaliyo na moshi ya wavutaji wa sigara na zaidi ya asilimia 70 kati yao hawakuwa na mtu katika familia yao ambaye amewahi kuugua maradhi ya asthma.

Watoto hao walilelewa kwenye mazingira yaliyokuwa na sabuni kwa muda wa miaka mitatu. Baadaye walipimwa kubaini ikiwa walikuwa na maradhi ya asthma au la.

Watafiti hao walibaini kuwa karibu asilimia 40 ya watoto hao walikuwa na ugonjwa wa asthma walipofikisha umri wa miaka mitatu.?Karibu ya asilimia 100 ya watoto waliopatikana na maradhi ya asthma walilelewa kwenye mazingira yaliyokuwa na sabuni ya kuoshea vyombo vya jikoni, kufulia nguo na kusafishia sakafu.

Asthma ni ugonjwa unaoathiri njia ya kutoa au kuingiza hewa kweye mapafu.?Njia ya kupitisha pumzi huwa nyembamba, hufura na kutoa kamasi jingi zaidi. Kamasi hilo humfanya mwathiriwa kupumua kwa shida na huanza kukohoa na kuhisi kuishiwa pumzi.

Wakenya zaidi ya milioni 4 wanaaminika kuugua maradhi ya asthma.?Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) Evanson Kamuri, idadi kubwa ya Wakenya wanaougua asthma wanapatikana katika maeneo ya mijini.

“Hii ni kwa sababu maeneo ya mijini yako na hewa chafu zaidi ikilinganishwa na maeneo ya vijijini. Hewa ya maeneo ya mijini inachafuliwa na viwanda, magari mengi, marundo ya takataka, kati ya mambo mengineyo,” anasema.

Ugonjwa wa asthma hauna dawa lakini dalili zake zinaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa. Ugonjwa huo unapotambuliwa mapema, makali yake yanaweza kupunguzwa.

Kwa kawaida waathiriwa wa asthma hutumia kifaa kinachojulikana kama ‘inhaler’ ili kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa jiji la Nairobi na mji wa Eldoret zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa asthma na wengi wa waathiriwa ni watoto wakati ya umri wa miaka 10 na 14.

Kulingana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Simon Fraser sabuni za unga au majimaji zinazotoa harufu ndizo zinahusishwa zaidi na maradhi ya asthma.

Watafiti hao wanasema watoto wa umri wa chini ya mwaka mmoja wako katika hatari kubwa ya kupatwa na asthma kwa sababu kinga zao za mwili zingali hafifu na mfumo wa upumuaji haujakomaa.

Watoto pia hutumia muda wao mwingi wakichezea vitu mbalimbali kama vile sabuni na kutambaa kwenye sakafu iliyosafishwa kwa sabauni.

“Tafiti za hapo awali pia zimewahi kuhusisha sabuni na maradhi ya kupumua hivyo hatukushangazwa na matokeo hayo,” wakasema watafiti hao.

Wataalamu wa afya wanasema kuwa baadhi ya aina ya sabuni zinatengenezwa kwa kemikali zinazojulikana kama formaldehyde na 1,4-dioxane, ambazo hudhuru mapafu. Asilimia 22 ya sabuni zinazotumiwa nyumbani zimesheheni kemikali zinazosababisha asthma.

Kemikali inayojulikana kama benzalkonium chloride, ambayo hupatikana katika sabuni za kuua bakteria pia husababisha asthma.?Kemikali nyingine inayojulikana kama borax au boric acid ambayo hupatikana kwenye sabuni inatatiza homoni mwilini.

Wataalamu wanashauri wazazi kuepuka kutumia sabuni zinazotoa harufu kama njia mojawapo ya kuwakinga watoto dhidi ya kupata asthma.

Wataalamu wa afya wanashauri watu kununua sabuni zisizo na kemikali ambazo si hatari kwa watoto kwa kusoma viungo vilivyotumiwa kuitengeneza.

Kulingana na madaktari, maradhi ya asthma hayawezi kuambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine.

“Ugonjwa wa Asthma unaweza kurithishwa kutoka kwa mzazi hadi kwa mtoto. Lakini hauwezi kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine. Kadhalika, ugonjwa huu hauna dawa mara nyingi mwathiriwa hupewa dawa ya kuutuliza tu,”anasema Dkt Torooti Mwirigi.

Mtu aliye na ugonjwa wa asthma anaweza kuhisi ugumu wa kupumua anapokuwa kwenye mazingira ya vumbi, moshi wa magari na manukato yenye harufu kali.

Mgonjwa wa asthma ambaye tayari ameonyesha dalili za kuwa na ugumu wa kupumua anaweza kusaidiwa kwa kumsihi kupumu kwa utaratibu.

Mletee mwathiriwa kifaa cha inhaler ambacho hutumika kusukuma dawa kwenye mapafu kupitia mdomoni.

Madaktari pia wanashauri kuwa unaweza kumketisha wima mwathiriwa na kulegeza nguo ili apate hewa ya kutosha.