Makala

AFYA: Madhara ya uvutaji sigara

June 1st, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

Kung’oka nywele

UVUTAJI sigara hudhoofisha kinga ya mwili na kisha kudhuru mizizi ya nywele. Halii hii husababisha kung’oka kwa nywele.

Magonjwa ya macho

Moshi wa sigara huwasha macho na pili kemikali zilizo ndani ya sigara hupita kwenye mishipa, damu na hatimaye kudhuru macho. Sigara pia husababisha kudhoofika kwa sehemu ya kati ya macho (retina) na hivyo kupunguza uwezo wa macho kuona vizuri na hata kutofautisha rangi.

Kukunjamana kwa ngozi

Kemikali zinazopatikana ndani ya sigara hupunguza uwezo wa ngozi kujirekebisha hivyo basi inaanza kuzeeka haraka na kupoteza uwezo wa kulainika. Mvutaji wa sigara huonekana mkongwe zaidi kuliko umri wake.

Saratani ya ngozi

Uvutaji sigara unasababisha saratani ya ngozi. Kemikali za sigara husababisha vidonda kwenye ngozi na ambavyo haviponi kwa urahisi. Baada ya muda, hugeuka kuwa saratani.

Magonjwa ya meno

Sigara hutatiza mdomo na kuongeza uchafu unaoganda kwenye meno hivi kusababisha kuoza kwa meno, harufu mbaya mdomoni na uchafu wa meno. Sigara pia hutatiza kupona kwa vidonda hasa baada ya kung’olewa kwa jino.

Magonjwa ya mapafu

Uvutaji wa siagara ndio sababu kubwa zaidi ya saratani ya mapafu. Pia husababisha kupasuka kwa vibofu vya hewa safi na kutoa harufu mbaya mwilini. Wavutaji pia hupata saratani ya koromeo na kuziba njia ya hewa na hivo basi inabidi kutobolewa kwa kishimo kwenye shingo hili kuwezesha mwadhiriwa kupumua.

Mifupa

Sigara inasababisha mifupa kuwa myepesi na kupunguza nguvu. Sababu ni kuwa kemikali zilizoko ndani ya sigara hupunguza uwezo wa mwili kujenga mifupa iliyo na nguvu.

Vidonda vya tumbo

Sigara hupunguza uwezo wa mwili kujikinga dhidi ya viini vinavvyosababisha vidonda tumboni. Pia hupunguza uwezo wa tumbo kustahimili nguvu ya asidi baada ya kula. Vidonda vya mvutaji basi huwa ni vigumu kutibu, na mara nyingi hutokea tena baada ya kupona.

Vidole

Kutu ya sigara hukusanyika na kuganda kwenye kucha na baina ya vidole vya mvutaji. Kisha hubadilisha rangi ya vidole na kucha kuwa za manjano au maji ya kunde. Ngozi ya vidole pia hukauka na kuwa ngumu sababu ya joto na kemikali za sigara.

Wanawake

Sigara huongeza hatari ya kupata saratani ya mfuko wa uzazi. Ni vigumu zaidi kwa mwanamke mvutaji sigara kutungwa mimba na ni rahisi sana kwake kumpoteza mtoto katika mimba.