Makala

AFYA: Manufaa ya juisi ya mua

May 27th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WATU wengi wanapenda vitu vitamu vyenye sukari.

Mua ambao ni mmea mwembamba na mrefu kama mwanzi – bamboo – huwa na majimaji yenye ladha tamu. Miwa hukuzwa kwa wingi katika kaunti za Kakamega, Busia, na Kisumu nchini Kenya.

Juisi ya mua inayotengenezwa kwa kuufinya na kutenganisha maganda, ina manufaa kadhaa mwilini.

Juisi hii ina uwezo mkubwa wa kuipa miili yetu nguvu kwa haraka na kukata kiu, na hii inasababishwa na sukari aina ya “sucrose” ambayo kazi yake kuu ni kuupa mwili nguvu. Ukiwa na uchovu, badala ya kunywa vinywaji vya viwandani tafuta juisi ya mua.

Juisi ya mua ni tamu lakini pia ni nzuri kwa wagonjwa wa kisukari kwa sababu ina sukari halisi ambayo ina uwezo mdogo wa kuzidisha kiwango cha sukari mwilini. Kutokana na hilo, juisi ya mua ndiyo anayoshauriwa mtu ainywe au aitumie badala wa vinywaji vingine.

Hii juisi ni muhimu ifahamike kwamba ina kiwango kikubwa cha madini ya calcium, magnesium, potassium, chuma na manganese. Madini ya potassium husaidia kuimarisha mmeng’enyo wa chakula.

Juisi ya miwa inasaidia kuongeza kiwango cha protini mwilini na kuimarisha ufanyaji kazi wa figo.

Ina jukumu kubwa la kusaidia kuzuia maambukizi katika tumbo na utumbo.

Aidha, ni suluhisho tosha na hutumika kutibu matatizo ya choo kigumu yaani “constipation”.

Juisi ya mua vilevile husaidia kuzuia meno kuoza na matatizo ya kupumua kutokana na kuwa na kiasi kikubwa cha madini.

Juisi ya miwa husaidia kung’arisha meno yako. Hivyo basi, ni muhimu kunywa juisi ya mua mara kwa mara.