Maradhi ya Trakoma yanapofusha maelfu maeneo kame

Maradhi ya Trakoma yanapofusha maelfu maeneo kame

Na LEONARD ONYANGO

VISA vya watu walio na matatizo ya macho vinaongezeka kwa kasi humu nchini kutokana na sababu mbalimbali.

Lakini jamii za wafugaji na wakazi wa maeneo kame, wanakabiliwa na tishio la upofu maradufu kutokana na kukithiri kwa ugonjwa wa trakoma (trachoma).Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa idadi ya Wakenya wanaoenda hospitalini kutafuta matibabu ya macho imekuwa ikiongezeka kila mwaka tangu 2016.

Watu milioni 1.1 walienda hospitalini kutafuta matibabu ya macho mwaka jana ikilinganishwa na milioni 1 mnamo 2019, kwa mujibu wa takwimu hizo.Wataalamu wanaamini kuwa idadi kubwa ya waliotafuta matibabu ya macho hospitalini walikuwa na ugonjwa trakoma.

Esther Saitoti, 65, mkazi wa Olturoto katika Kaunti ya Kajiado, amekuwa akihangaishwa na matatizo ya macho kwa zaidi ya miaka mitano. Lakini angali ana matumaini kwamba siku moja atapata matibabu na macho yake kuona vizuri.

Bi Saitoti anasema kuwa alipimwa mapema mwaka huu na kuelezwa kwamba alikuwa na ugonjwa wa trakoma lakini hakufanyiwa upasuaji kutokana na ukosefu wa fedha.“Nimekuwa nikisumbuliwa na macho kwa muda mrefu.

Kope (nywele za machoni) huingia ndani ya macho mara kwa mara na kunisababishia maumivu makali. Mjukuu wangu amekuwa akinisaidia kuondoa nywele hizo ndani ya macho kwa kunipuliza. Lakini sijawahi kupata afueni,” anasema.

Bi Saitoti, hata hivyo, ana bahati kwani hajapofuka – macho yake yatapona iwapo atapata matibabu ya haraka kabla ya kuathiriwa kabisa na maradhi haya. Wakenya zaidi ya 53,000 wamepofuka kutokana na maradhi ya trakoma – ambayo kulingana na wizara ya Afya yamekithiri zaidi katika kaunti 12.

Ripoti ya Sensa ya 2019, inaashiria kwamba Wakenya 333,500 wana shida ya matatizo ya macho na kati yao 259,000 wanaishi katika maeneo ya vijijini.Trakoma ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria wanaojulikana kama Chlamydia trachomatis.

Bakteria hao hushambulia sehemu ya ndani ya jicho na kusababisha kidonda chenye uchungu kinachojeruhi sehemu ya inayojulikana kama konea(cornea).Ugonjwa huo unaongoza kwa kusababisha upofu kote ulimwenguni.

Ni miongoni mwa maradhi 20 yaliyoorodheshwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuwa yametelekezwa. Magonjwa hayo hayajapewa kipaumbele licha ya kuhangaisha mamilioni ya watu duniani.

Mkuu wa kitengo cha maradhi yaliyotelekezwa katika wizara ya Afya, Dkt Wycliffe Omondi, anasema kuwa zaidi ya watu milioni 11 wako katika hatari ya kupatwa na trakoma.Kaunti za Turkana, Baringo, Pokot Magharibi, Isiolo, Marsabit, Wajir, Narok, Kajiado, Meru, Embu, Kitui na Laikipia zinaongoza kwa visa vingi vya maambukizi nchini.

Kaunti ya Turkana, kwa mfano, maambukizi ni asilimia 42, kulingana na utafiti uliofanywa hivi karibuni.Dkt Omondi anasema kuwa mwaka huu serikali inalenga kutibu wagonjwa milioni 2.8 katika Kaunti za Baringo, Isiolo, Kajiado, Narok, Samburu, Turkana na Pokot Magharibi.

Wizara ya Afya inakadiria kuwa jumla ya waathiriwa 5,000 wanafaa kufanyiwa upasuaji wa dharura ili kuwaepusha kupofuka.Wiki iliyopita, Kenya na Uganda zilitia saini mkataba wa kukabiliana na maradhi haya katika eneo la mpakani.

Wachungaji wa mifugo kutoka pande zote wamekuwa wakiambukizana wanapovuka mpaka kutafuta malisho hivyo kuwa vigumu kukabiliana na maradhi haya.“Bakteria wanaosababisha trakoma wanaenezwa kupitia nguo chafu, mikono, malazi machafu na jamii zinazoishi kwenye maeneo yaliyo na uhaba wa maji.

Nzi waliogusa majimaji yanayotoka kwenye macho au pua ya mwathiriwa pia husambaza ugonjwa huu,” anasema Dkt Omondi. Dkt Peter Ekwum, daktari wa macho, anaeleza kuwa upofu unaoletwa na trakoma unaweza kuzuilika iwapo utatibiwa mapema.“Hata hivyo, mtu akishapofuka kutokana na trakoma hawezi kusaidiwa kuona tena.

Huwa kipofu maisha yake yote. Siri ni kutafuta matibabu ya haraka kabla ya kupofuka,” anasema Dkt Ekwum.Anasema kuwa mwathiriwa, anapopepesa macho, kope hukwaruza konea. Sehemu hiyo ya jicho ikikwaruzwa kwa muda mrefu hubambuka na kuacha kidonda.

Dalili nyingine za ugonjwa huu ni kuwasha kwa macho, kutoka kwa usaha, kufura kwa kope, maumivu unapotazama kwenye mwangaza, uchungu, kuhisi ukavu machoni na hata kushindwa kuona.“Kidonda hicho huwa na uchungu mwingi na hata ingawa mtu hupona baada ya muda, jeraha hubaki pale.

Kuambukizwa ugonjwa huo mara kwa mara kunamfanya mtu kupata matatizo ya kuona na mwishowe kupofuka,” akaeleza Dkt Ekwum.Dkt Omondi anasema kuwa ugonjwa huu unahangaisha zaidi watoto na wanawake.

“Hii ni kwa sababu watoto hutembea na uchafu machoni kwa muda mrefu. Wadudu walio na bakteria wanaoambukiza trakoma wanapotua kwenye uso wa mtoto, humfanya kupatwa na maradhi haya. Wanawake pia hutangamana na watoto zaidi kuliko wanaume hivyo kuongeza uwezekano wa kuambukizwa,” anasema.

Matibabu

Ugonjwa huu hutibiwa kwa kutumia tembe za Zithromax zinazoua bakteria wa Chlamydia trachomatis.Kenya imekuwa ikipokea tembe hizo kutoka kwa Mpango wa Kimataifa wa Kupambana na Trakoma (ITI).

Kenya imepokea tembe za jumla ya Sh15 milioni kutoka kwa ITI tangu 2007. Mapema mwaka huu, serikali na ITI ilitia saini mkataba wa makubaliano ili kupata dawa za trakoma kwa miaka mitatu ijayo.

Lakini Dkt Omondi anasema kuwa mengi zaidi yanafaa kufanywa kupambana na maradhi haya mbali na kutoa tembe. “Kuwapa watu dawa kunafaa lakini hakutasaidia kuangamiza maradhi haya. Jamii zilizoathiriwa zinafaa kupewa maji safi kama njia mojawapo ya kupunguza maambukizi,” anasisitiza.

Mnamo mwaka wa 1998, Baraza la Afya la Umoja wa Mataifa lilizindua azimio la WHA51.11 lililonuia kuondoa ugonjwa wa trakoma kwenye orodha ya magonjwa yanayodhuru afya za umma kabla ya mwaka 2020.

Kenya ilinuia kuangamiza trakoma kufikia 2020 lakini ikashindwa mpango huo ulipogonga mwamba. Kenya sasa inalenga kuangamiza maradhi haya kufikia 2023.Watu milioni 1.9 wamepofushwa na trakoma kote ulimwenguni, kwa mujibu wa WHO.

Trakoma huchangia asilimia 1.4 ya upofu ulimwenguni.Shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN) linasema kuwa nchi 44, ikiwemo Kenya, zimeathirika zaidi. WHO ilitangaza mataifa 13 yaliyofikia malengo ya ugonjwa wa trakoma Septemba 2020.

Mataifa hayo yalikuwa China, Gambia, Cambodia, Ghana, Iran, Iraq, Mexico, Morocco, Myanmar, Nepal, Oman na Togo.Mkurugenzi wa ITI Afrika, Dkt Teshome Kanno wiki iliyopita alizitaka serikali za kaunti zilizoathirika kushirikiana na serikali ya kitaifa kupambana na ugonjwa huu bila kuingiza siasa.

You can share this post!

Dawa mpya yathibitishwa kuwa na uwezo wa kupunguza makali...

Wanajeshi wapindua serikali ya muda Sudan

F M