Makala

AFYA: Miaka 17 baadaye bado chozi linamtiririka…

October 26th, 2020 4 min read

NA PAULINE ONGAJI

Kwa miaka 17, maisha ya Risper Muhoma, 40, mkazi wa kitongoji duni cha Kibra, jijini Nairobi, yamekuwa magumu.

Katika muda huu wote, Bi Muhoma na mumewe, wamekumbwa na mzigo wa kumlea mtoto wao wa pili, Vincent Wanga, ambaye alizaliwa akiwa na utindio wa ubongo (Cerebral Palsy).

“Pindi baada ya kumzaa, tulitambua kwamba alikuwa na matatizo kwani hangeweza kunyonya vizuri. Baada ya kumpeleka hospitalini, madaktari waligundua kwamba alikuwa na utindio wa ubongo,” aeleza.

Tangu azaliwe, Vincent hajawahi kuzungumza, huku miguu na mikono yake ikiwa imelegea ambapo anategemea hasa kiti cha magurudumu kusonga. Aidha, mikono yake ni dhaifu kiasi kwamba hawezi jifanyia chochote.

“Tangu awe na miaka sita, amekuwa akipokea tiba ya maungo katika kituo cha Mary Rice Center, Kibra ambapo polepole alijifunza kujifanyia mambo madogo madogo kama vile kula, kuzungumza, kuvua na kuvaa nguo,” asema.

Lakini licha ya hayo, mazungumzo na uwezo wake wa kutembea na kutumia mikono yake kikamilifu bado ni dhaifu, kumaanisha kwamba lazima kuwe na mtu wa kumshughulikia kila wakati.

“Pia, lazima atumie kiti cha magurudumu ambacho kwa sasa hana, kwani alichokuwa nacho kiliungua nyumba yetu ilipoteketea miaka miwili iliyopita. Kwa hivyo ili kusonga kutoka sehemu moja hadi nyingine, inabidi atambae, kumaanisha kwamba bado anategemea usaidizi wangu pakubwa,” aeleza.

Huu ni mzigo mzito hasa kwa Bi Muhoma ambaye kama mama, yeye ndiye hukumbwa na jukumu kubwa la kumshughulikia mtoto huyu, vile vile wanawe wengine wanne, mumewe akiwa kazini.

Anasema kwamba mzigo wa kumlea mwanawe mlemavu umekuwa mzito kiasi cha kutostahimilika. “Nampenda sana lakini tangu mtoto huyu azaliwe, maisha yangu yamebadilika. Ilinilazimu kukatiza ndoto zangu ili nimshugulikie,” asikitika.

Pia, kama mlezi wake mkuu, kwa miaka hii yote amelazimika kustahimili unyanyapaa, kutengwa, kutukanwa na hata kulazwa hospitalini kutokana na msongo wa mawazo.

“Nimekumbana na watu ambao wamehusisha hali ya mwanangu na laana au uchawi. Hasa mwanzoni mambo yalikuwa magumu zaidi ambapo mara nyingi nilijipata nikilia. Kuna wakati nililazwa hospitalini kwa mwezi mmoja kutokana na msongo wa mawazo uliosababisha nishindwe kuzungumza,” aongeza.

Hali hii pia imekuwa na athari kubwa kwa maisha yao kifedha. “Kwa mfano, pindi alipozaliwa na kutambuliwa kuugua maradhi haya, mume wangu naye akaachishwa kazi kutokana na mazoea aliyokuwa nayo ya kuomba ruhusa kila wakati ili tumpeleke hospitalini. Tangu wakati huo, amekuwa akitegemea vibarua,” aeleza.

Maisha yamekuwa magumu hata zaidi wakati huu wa janga la Covid-19. “Kuna nyakati ambapo ningejikakamua na kufanya vibarua vya kufua nguo, lakini kwa sasa havipatikani. Aidha, mume wangu ambaye tegemeo lake limekuwa vibarua vya sulubu, hana riziki kwa sasa kwani kazi hizo hazipatikani.”

Katika haya yote, Bi Muhoma na mumewe, kama wazazi na walezi wa mtoto mwenye ulemavu wa kiakili wamekuwa, wakipambana bila ushauri nasaha au usaidizi mwingine wa kisaikolojia.

“Ni wakati mmoja tu ambapo nilipata mafunzo kupitia warsha moja niliyoalikwa, ambapo tulipewa mafunzo mbalimbali kuhusu jinsi ya kuwashughulikia watoto hawa na kuwakubali,” asema.

Bi Muhoma anawakilisha asilimia kubwa ya wazazi wanaowalea watoto wenye ulemavu wa kiakili hapa nchini, pasipo kupokea ushauri nasaha wa aina yoyote.

Kulingana na wataalamu wa kiafya, hii inahatarisha maisha sio tu ya mtoto mwenye ulemavu, bali pia hali ya kiakili ya mzazi.

Dkt Lincoln Kasakhala wa Idara ya tiba ya magonjwa ya akili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, asema ushauri nasaha kwa mzazi anayemlea mtoto anayekumbwa na matatizo ya kiakili ni muhimu kwa sababu changamoto wanazokumbana nazo ni nyingi.

“Mara nyingi wazazi hawa huelekeza mawazo yao kwa mahitaji ya watoto hawa na vile vile majukumu mengine yanayowakabili na hao wenyewe kujisahau. Wengi wa wazazi hawa hawana muda wa kufanya mambo yao wenyewe kujifurahisha,” anasema

Dkt Kasakhala asema, hasa kwa watoto wanaougua utindio wa ubongo, changamoto kuu inayowakumba wazazi hawa ni jinsi ya kudhibiti tabia zao.

“Kuna wazazi wanaoona aibu kwa kutokuwa na uwezo wa kudhibiti tabia ya watoto wao katika maeneo ya umma na ili kuepuka hili, wanaonelea heri kujitenga,” anasema.

Ni suala linalowafanya wazazi hawa kutengwa na wenzao, familia na jamii kwa jumla, ambapo ni rahisi kwa mwanamume kutoroka na kumuacha mama akimlea mtoto kivyake.

Aidha, anasema wazazi hawa hukumbwa na matatizo ya kifedha kwani ni gharama kubwa kumlea mtoto anayekumbwa na ulemavu huu.

“Huduma kwa watoto wanaokumbwa na hali hii hazipatikani kwa urahisi hasa katika maeneo ya mashambani. Na hata mijini, huduma hizi zinapopatikana, wazazi wengi hawawezi kumudu. Aidha, jamii nyingi huwatenga wazazi wa aina hii, suala linalowafanya wengi wasijitokeze ili watoto wao wapate usaidizi,” aongeza.

Kwa wale wasioweza kumudu huduma hizi, mambo huwa mabaya kwani kuna hatari ya mzazi huyu kuhisi kana kwamba amefeli au ni makosa yake, suala linalowafanya kupoteza matumaini.

Mtaalamu huyu anasema kwamba hii ni hatari kwani kutokuwa na uwezo wa kufikia rasilmali za matibabu au ukosefu wa ufahamu huwasababishia wasiwasi, kupoteza matumaini na mawazo mengi, hali ambayo yaweza kuwaathiri kiakili kabisa.

“Wakati huu ni rahisi kwao kuanza kujilaumu na kukumbwa na hasira, ambapo kinachofuatia ni msongo wa akili. Mambo yakifikia hapa, sasa wataanza kuonyesha ishara kama vile kukosa usingizi, kukosa hamu ya kula, matatizo ya kumakinika na hivyo ugumu wa kufanya maamuzi, uchovu na maumivu ya mwili.

Dkt Kasakhala anasema kuna hatari ya mzazi huyu kukumbwa na hisia za kumuua mtoto huyu au yeye mwenyewe kujiua.

Lakini licha ya umuhimu wa matibabu haya miongoni mwa wazazi wa watoto hawa, asema kwamba hapa nchini bado ni changamoto.

“Ikiwa mtoto anaugua utindio wa ubongo, mzazi ana mahitaji tofauti ya ushauri nasaha. Katika kila awamu ya kukua, mtoto huyu atakuwa na mahitaji tofauti, kumaanisha kwamba lazima mzazi naye pia apokee ushauri tofauti wakati huu,” asema.

Kulingana naye, kuna hospitali za umma zinazotoa huduma hizi lakini bado kiwango cha mahitaji kiko juu. “Kwa upande mwingine, huduma hizi katika taasisi za kibinafsi zaweza kufikia Sh2, 000 kwa kila kipindi cha ushauri nasaha, kulingana na umri wa mtoto. Sio wazazi wengi wanaoweza kumudu gharama hii,” aongeza.

Japo kumekuwa na jitihada za kuhakikisha huduma za ushauri nasaha kwa wazazi hawa zinatolewa kwa viwango vya kaunti, mtaalamu huyu asema, kibarua kikubwa ni kuhakikisha kwamba wazazi hawa wanajitokeza na kupokea usaidizi.

Aidha anasema kwamba, pasipo usaidizi wa kijamii, kuna uwezekano mkubwa wa wazazi hawa kuathirika kiakili. “Kama jamii tunaweza ingilia kati. Kwa mfano, mbali na kuchangia kifedha kuhakikisha kwamba mzazi anaweza kumudu gharama ya kukidhi mahitaji ya mwanawe, unaweza jitolea muda wako na kumsaidia kumshughulikia mwanawe mara kwa mara, angalau naye apate fursa ya kwenda kazini au kupumzika,” asema.

Kwa upande mwingine anasisitiza umuhimu wa wazazi wahusika nao kutafuta usaidizi kupitia makundi tofauti ya kutoa usaidizi kwa watoto wanaougua maradhi ya aina hii. “Kwa mfano, kuna mashirika ambayo mbali na kusaidia wahusika kupokea tiba, mara nyingi huandaa warsha na vikao ambapo wanapata fursa ya kukutana na kuzungumzia changamoto zao na kusaidiana,” ahitimisha.