AFYA: MKU yazindua kituo cha wahadhiri, wanafunzi kufanyia mazoezi

AFYA: MKU yazindua kituo cha wahadhiri, wanafunzi kufanyia mazoezi

Na LAWRENCE ONGARO

CHUO Kikuu cha Mount Kenya (MKU) kimezindua kituo cha kisasa cha kufanyia mazoezi kwa wanafunzi na wahadhiri.

Mwanzilishi wa chuo hicho Prof Simon Gicharu, alisema hiyo ni hatua kubwa ambayo chuo hicho imepiga na itanufaisha watu wengi kiafya.

“Tunaelewa vyema ya kwamba mtu anayezingatia mazoezi huwa na afya njema huku akiepukana pia na maradhi tofauti mwilini,” alisema Prof Gicharu.

Alisema kukiwa na watu wengi wenye afya njema hata bima ya afya itapungua kwa kuwa idadi ya watu wengi ambao watakuwa timamu kiafya na kimwili.

Alieleza hii ni hatua mojawapo ya maendeleo makubwa ya kujivunia ambayo chuo hicho kimefanya kwa kuzingatia afya ya wanafunzi, wahadhiri na hata wafanyakazi wote walioko huko.

“Chuo chetu kimepata sifa tele kwa kuzingatia maswala ya spoti kwa sababu wanafunzi wengi wanashiriki katika michezo tofauti ikiwemo soka, karate, vikapu, na voliboli miongoni mwa mingine.

Alisema anampongeza Dkt Peter Kirira ambaye ndiye alitoa pendekezo la kituo hicho kujengwa ili kunufaisha wanafunzi na wahadhiri kwa mazoezi yao ya kila mara.

“Kulingana na utafiti, mwili huwa katika hali nzuri hasa ukizoeshwa mazoezi ya muda wa saa tatu mara tatu kwa wiki moja. Ni bora kufanya hivyo kuepuka maradhi mengi yanayochipuka kila mara,” alisema Prof Gicharu.

Naibu chansela wa chuo hicho, Prof Deogratius Jaganyi alisema kituo kingine kinapangwa kujengwa hivi karibuni katika bewa la MKU lililoko Kigali nchini Rwanda.

Alisema MKU pia inazidi kuendeleza masomo ya uandishi na uanahabari kupitia kituo cha TV-47 na Royal FM Radio ya Rwanda.

Alisema chuo hicho pia kinajivunia kuwa na wanafunzi wawili waliopokea ufadhili kutokana na ubunifu wao wa kikazi.

Bw Christopher Mwanza Arunga alipokea ufadhili wa Sh3.6 milioni kwa kubuni mtambo wa kuunda chakula cha mifugo Kaunti ya kakamega. Naye Sylvia Wanjiku alipokea ufadhili wa laki tisa – Sh900,000 baada ya kubobea kwa utengenezaji wa chokoleti.

Aliwapa changamoto wanafunzi wa chuo hicho wawe mstari wa mbele kuwa wabunifu ili nao waweze kupokea msaada huo wa ufadhili.

You can share this post!

Beki Eric Garcia abanduka Man-City na kutua Barcelona kwa...

Barcelona wampa Messi mkataba mpya wa miaka miwili