Makala

AFYA NA ULIMBWENDE: Ujauzito haumaanishi kupoteza mvuto

October 19th, 2020 2 min read

Na MARGARET MAINA

ZIPO njia mbalimbali za kukusaidia kufurahia urembo wako mwanamke hasa katika kipindi maalumu maishani mwako; ujauzito.

Kunywa maji

Kipindi cha ujauzito unahitajika kunywa maji mengi kwa siku. Yatakusaidia kusafisha na kutoa taka na sumu mwilini mwako. Maji ni muhimu zaidi kwa afya yako na mwana wako mtarajiwa. Kunywa angalau lita mbili za maji kwa siku.

Mlo sahihi

Unahitaji uangalizi na umakini wa ziada katika chakula unachokila wakati wa ujauzito ili kuilinda na kuimarisha afya yako. Unashauriwa kumhusisha daktari wako au mtaalamu wa lishe kukuandalia ratiba ya aina ya chakula unachotakiwa kula. Fuatilia ratiba hii kwa umakini, kula kwa afya; ikiwa pia ni muhimu kwa ajili ya mtoto wako.

Pata muda wa kulala

Hali ya uchovu ni dalili mojawapo anazopata mama mjamzito hasa katika kipindi cha mwanzo. Kupumzika vizuri ni muhimu kwa ajili ya mwili na akili yako mwenyewe. Hakikisha unapata muda mzuri na wa kutosha kupumzika kiasi kwamba mwili wako uwe unahisi uchovu kidogo. Jiweke huru wakati wa kulala. Hakikisha unapumzika pahala pazuri; unaweza kutaka kutumia mito au kitu kingine kama takia ili ujihisi mwepesi.

Uzani sahihi

Unahitajika kuangalia uzani wako kipindi cha ujauzito. Baadhi ya akina mama wanakula chochote na kila kitu pasipo kuhofia kuhusu uzani. Ikiwa ni kawaida kuongezeka uzani wakati wa ujauzito, si vema kiafya kupitiliza viwango. Uzani unaongezeka kwa kula vyakula ambavyo havina msaada mwilini. Mara kwa mara kula mlo sahihi. Unaweza kumhusisha daktari wako ili kupata chaguo bora.

Mazoezi

Mazoezi ni muhimu. Kuna mazoezi maalumu kwa ajili ya wajawazito. Hudhuria darasa la mazoezi ya yoga yaliyoandaliwa kwa ajili ya wajawazito, pata muda wa kukutana na wajawazito wengine na kujifunza na kupata uzoefu. Unaweza pia kumuomba ushauri daktari ni michezo gani unaweza kushiriki.

Epuka michirizi

Akina mama wengi wanalalamika kupata michirizi baada ya kujifungua. Kuwa mwangalifu ili kuepuka hali hii kuanzia kipindi cha ujauzito. Tumia krimu uliyoshauriwa au zinazouzwa kwa ajili ya kuondoa michirizi. Tumia kila siku kuukanda mwili wako. Aghalabu kwa muda mfupi jiepushe na kukimbia au kuruka kama njia ya kuepuka michirizi.

Itunze ngozi yako

Pamoja na yote wakati wa ujauzito, usisahau ngozi yako. Urembo katika kipindi cha ujauzito unahusisha mwonekano wa ngozi. Kutokana na mabadiliko ya homoni kunaweza kuwa na athari katika ngozi yako. Unaweza kutumia bidhaa za kutunza ngozi kwa kuzingatia aina ya ngozi yako, lakini hakikisha hutumii kemikali hatarishi.

Vipodozi

Kutokana na mabadiliko ya homoni, unaweza kupata madoa usoni. Vipodozi ndivyo mkombozi; tena angalia zile bidhaa ambazo hazitumii au hazitokani na kemikali kali.

Pumzika

Mwisho na muhimu zaidi ni; kukumbuka kupumzika. Lala chini kwa muda unapopata nafasi. Pumzisha mwili wako.