Makala

AFYA NA ULIMBWENDE: Vyakula vitakavyokuza nywele zako

May 14th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

KUWA na nywele zenye afya nzuri ni muhimu kwa wote bila kujali jinsia.

Hii ndiyo sababu baadhi ya watu huenda wakawa wanatumia dawa za aina mbalimbali za kuhakikisha nywele zao zinastawi na kuwa na mwonekano mzuri.

Lakini wengi wanaotumia dawa zinazotengenezwa kwa kemikali hujikuta katika wakati mgumu baada ya kuzitumia kwa muda kwani hukabiliwa na matatizo ya nywele kukatika na hata kupata madhara katika ngozi ya kichwa.

Njia bora na salama zaidi ya kustawisha nywele na kuzifanya ziwe na mvuto wa aina yake ni kula vyakula vyenye virutubisho muhimu kwa afya ya nywele.

Yai

Nywele za binadamu zina protini.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa zina protini ya kutosha, na hilo hufanyika kupitia vyakula.

Protini ni nguzo kuu ya nywele za binadamu, na yai ni moja kati ya vyakula vyenye utajiri mkubwa wa protini.

Hakikisha unakula yai angalau mara tatu kwa wiki.

Mchicha

Nywele zinahitaji madini ya chuma ili ziweze kuwa katika hali nzuri kiafya. Kukosekana kwa madini ya chuma husababisha nywele kunyonyoka.

Mwili unapokosa madini ya chuma, hewa ya oksijeni na virutubisho hushindwa kufika vizuri kwenye mizizi ya nywele hivyo hufanya nywele kuwa dhaifu na zisizo na mwonekano mzuri.

Mboga za majani aina ya mchicha ni suluhisho, kwa kuwa zina madini ya chuma kwa wingi ambayo seli za nywele huhitaji.

Limau na machungwa

Mwili wa binadamu huhitaji vitamini C ambayo husaidia kuhuisha utendaji wa madini ya chuma. Hivyo, unapaswa kuongeza matunda ya jamii ya ‘citrus’ kama vile machungwa na limau. Pia, unaweza kutumia na asali pamoja.

Vitamini C husaidia katika ukuaji wa nywele, kusaidia usambaaji wa virutubisho na ukuaji wa haraka wa nywele.

Karoti

Karoti. Picha/ Maktaba

Ni muhimu sana kuhakikisha unakunywa juisi ya karoti kila siku kama unataka nywele zako zikue haraka zikiwa na mwonekano mzuri wenye afya.

Vitamini A inayopatikana kwenye karoti ni muhimu sana kwa ukuaji wa seli za nywele.

Karoti ina mafuta asili yanayofahamika kama ‘sebum’ na mizizi ambayo husaidia kukuza nywele kwa haraka.

Parachichi

Tunda aina ya parachichi lina kazi nyingi sana mwilini kama matunda mengine, lakini hili ni tunda la kipekee ambalo lina utajiri wa vitamini E ambayo husaidia mzunguko wa damu na katika hilo husaidia mfumo wa ukuaji wa nywele kwa haraka.

Tunda hili husaidia kuhuisha na kurekebisha mafuta na kiwango cha pH (inayosafisha kemikalii mwilini); vitu ambavyo kama vitazidi kwenye mwili vinaweza kusababisha kusimama kwa ukuaji wa nywele.

Kwa faida zaidi, vitamini E inayopatikana kwenye parachichi kwa wingi husaidia zaidi afya ya moyo wa binadamu na zaidi ngozi.

Hivi ni baadhi tu ya vyakula na matunda kwa ukuaji mzuri wa nywele zako.