Makala

AFYA: Umuhimu wa kufanya mazoezi asubuhi

July 4th, 2019 2 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

WAKATI tatizo la unene kupindukia (obesity) likiongezeka katika jamii zetu, watu wengi wenye tatizo hili wamekuwa wakihangaika hapa na pale bila kujua njia mojawapo ya kulikabili ni kufanya mazoezi.

Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha mtu kutofanya mazoezi. Baadhi yazo ni maradhi aliyo nayo mtu, kutoyapa mazoezi ya mwili kipaumbele, ukosefu wa maarifa na kadhalika.

Mtu anahitajika kujitahidi kunufaika kutokana na mazoezi.

Mazoezi husaidia kuimarisha siha ya mtu

Kukimbia angalau muda wa saa chache kwa wiki kutakufanya uwe mchangamfu na kuimarisha utendakazi wako. Hivyo mtu anakuwa bila mawazo hasi yanayoweza kudhoofisha afya.

Huimarisha moyo na mapafu

Kwa mtu wa kawaida, mwili hutumia hewa aina  ya oksijeni mara 10 zaidi wakati wa kufanya zoezi rahisi la kukimbia ukilinganisha na akiwa amekaa.

Mtu anapofanya zoezi huimarisha mfumo wa moyo wa usukumaji damu hivyo moyo na mapafu pia hufanya kazi zake kwa ufanisi.

Huboresha utendaji kazi wa ubongo na kuongeza uwezo wa mtu kufikiri

Pamoja na kwamba mazoezi yana manufaa mengi kiafya, pia inaaminika mazoezi ya kukimbia husababisha ubongo kuzalisha homoni iitwayo “endorphin’’ ambayo huibua hisia za furaha na kumfanya mtu awe katika hali ya kuwa na raha na mwenye mawazo mazuri.

Sio tu kwamba mazoezi haya yatakufanya ujihisi kuwa katika hali ya furaha kwa muda bali yatakufanya pia uongeze ujasiri wako wa kujiamini na kujikubali mwenyewe. Hapo utapunguza msongo wa mawazo na matatizo mengine yanayosababishwa na kuchoka kwa ubongo.

Hupunguza uzani wa mwili na mafuta mwilini

Sote tunajua unapofanya mazoezi, baada ya muda utajisikia mchovu kwelikweli ambapo unatokwa na jasho, kuhema sana na kadhalika. Haya yote ni matokeo baada ya kufanya zoezi la kukimbia. Unapofanya maozezi, unachoma kalori ‘calories’ mwilini na hatimaye kupunguza mafuta.

Ikiwa utakuwa unafanya mazoezi ya kukimbia ipasavyo na kwa malengo, ni rahisi kwako kuona mabadiliko ya mwili wako baada ya wiki chache.

Kama wewe ni mnene na una uzani mkubwa wa mwili, huu ndio wakati wako wa kuanza kufanya mazoezi ya kukimbia.