AFYA: Umuhimu wa mazoezi kwa wajawazito

AFYA: Umuhimu wa mazoezi kwa wajawazito

Na MARGARET MAINA

mwmaina@ke.nationmedia.com

MAMA mjamzito anashauriwa afanye mazoezi mepesi angalau kila siku katika kipindi chake chote cha ujauzito.

Ikilinganishwa na miongo kadhaa hapo nyuma, nyakati hizi wajawazito wengi wamekuwa wakishauriwa na wataalamu wa afya kujihusisha na swala zima la ufanyaji wa mazoezi. Mazoezi huimarisha afya ya mama pamoja na mtoto.

Hivyo, ni vyema mama mjamzito kufanya mazoezi ya mwili na kuweka misuli sawa wakati wa ujauzito wake na hata baada ya kujifungua kwani hii humjengea afya bora ikiwa ni sambamba na kula mlo kamili. Kupitia mazoezi haya, afya ya mama na mtoto aliyeko tumboni huimarika maradufu.

Wataalamu hushauri mazoezi madhubuti yafanyike kwa muda kati ya dakika 10 mpaka nusu saa mimba isiwe na matatizo mengineyo yoyote yale. Pia mazoezi haya madhubuti kabisa ni muhimu sana kwa wajawazito ambao shughuli zao za kila siku sio za kutosheleza kuifanya miili yao kuwa katika ubora unaohitajika.

Mazoezi yapo ya aina nyingi sana ambayo mtu wa aina yeyote ile anaweza kuyafanya na yakamsaidia kulinda na kujenga afya imara. Lakini mazoezi haya hutegemea na umbile ama umri wa mtu.

Mama mjamzito anaweza kufanya mazoezi ya kutembea au kukimbia taratibu, lakini pia kama ni mpenzi wa kuogelea, basi ni mojawapo ya mazoezi mazuri yanayopendekezwa na wataalamu wengi wa maswala ya wanawake. Wengi hupenda aina hii ya mazoezi kwani ni rahisi mno kwa kunyoosha viungo vya mwili.

  • husaidia kujenga na kuimarisha afya ya mama na mtoto
  • kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kisukari cha ujauzito na shinikizo la damu
  • pia hupunguza uwezekano wa kupasuliwa wakati wa kujifungua

Wakati wa mazoezi, ni vyema ukawa makini na aina ya zoezi unalolifanya kusudi lisije likawa na madhara kwako na kwa mtoto. Jiepushe na michezo ya kugusana kama mpira na mingine yote iliyo kwenye kategoria hiyo.

Pia vaa viatu vyenye visigino vifupi – short heels – wakati wa mazoezi. Pia visiwe na soli inayoweza kufanya uteleze kwa urahisi. Epuka michezo ya kuzama majini wakati wa ujauzito kwani ni hatari sana. Pia kupanda milima mirefu ni hatari kwa afya yako na mtoto.

You can share this post!

Mahabusu alalama Kortini hakupewa chakula akiwa rumande

Athari za kutumia vyombo na bidhaa za plastiki