Dondoo

Ageuza chumba danguro, sasa amlaumu jirani

May 15th, 2019 1 min read

Na DENNIS SINYO
SHINYALU,KAKAMEGA
KIOJA kilitokea hapa polo alipomkemea vikali jirani yake akimlaumu kwa kutaka kuharibu ndoa yake.
 
Jamaa alidai kwamba jirani alimsengenya kwa mkewe.
Yasemekana jamaa alikuwa na tabia ya kufika nyumbani akiwa na vipusa jambo ambalo jirani yake hakufurahia. Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa akibadilisha vipusa kila wikendi.
Baadhi ya wapangaji kwenye ploti walianza kuwa na maswali mengi kutaka kujua iwapo jamaa alikuwa ameoa au la.
 
Hata hivyo, mambo yalichukua mkondo mwingine mama mmoja alipowasili kwenye ploti na kusema alikuwa mke wa jamaa. Kila mtu alipigwa na butwaa kujua jamaa alikuwa ameoa.
Mama huyo alianza kupiga gumzo na mama mmoja aliyejitambulisha kuwa jirani wa jamaa kwenye ploti.
Mke wa jamaa alishtuka kusikia kwamba mumewe alikuwa amebadilisha nyumba yake kuwa danguro kwa kukaribisha vipusa kila wiki.
Polo hakuamini aliporejea jioni kutoka kazini na kukuta mkewe akiwa amefika. Yasemekana mama alianza kumtusi jamaa akidai alikuwa amemuacha ocha ili kupata nafasi ya kuponda raha na viruka njia wa mjini.
“Kila mara unasema kazi ni nyingi, kumbe haja yako ni kuponda raha na hawa wasichana?’’alifoka mama huyo.
Baada ya jamaa kufaulu kumshawishi mkewe kurejea kijijini, alimgeukia jirani yake na kumtusi, akimlaumu kwa kumharibia ndoa.
“Kwani wewe ni mama wa aina gani? Unanichomea picha mbele ya mke wangu kwa sababu gani? Badala ya kushughulika na mambo yako unampa mke wangu udaku ufaidike na nini?’’ polo alichemka.
Mama huyo alifyata mdomo kwa dakika chache kabla ya kudai kwamba hakusema chochote kisicho cha kweli. Siku iliyofuatia, jamaa alihamia ploti nyingine.