Agizo aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha wazazi afike kortini

Agizo aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha wazazi afike kortini

NA RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu imemwagiza aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha kitaifa cha wazazi (NPA), Bw Nicholas Maiyo, afike kortini Oktoba 6, 2022 kujitetea kwa kupuuza agizo la korti kuwa ang’atuke afisini.

Bw Maiyo na maafisa wengine wa zamani wa NPA waliamriwa Septemba 19, 2022, wang’atuke afisini na Jaji Hedwiq Ong’udi kwa sababu walichaguliwa kwa njia isiyo halali.

Jaji Ong’udi alimwamuru Bw Maiyo na wenzake wawakabidhi afisi maafisa wapya wa NPA wakiongozwa na Bw Sila David Obuhatsa, lakini amekataa kuondoka.

Akiwasilisha ombi la kumsukuma gerezani Bw Maiyo, wakili Njeri Ngunjiri alieleza Jaji Mugure Thande, kwamba mshtakiwa (Maiyo) na wenzake wameidharau mahakama na wanastahili adhabu kali.

Bi Ngunjiri aliomba jaji amwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi awakamate Bw Maiyo, Jeremiah Nyakundi na Sarah Kagendo Mitambo na kuwafikisha kortini ili wasukumwe magereza ya Viwandani na Lang’ata.

“Hii mahakama inafaa kuwaadhibu washtakiwa kwa kuidharau na kukaidi maagizo waondoke afisini,”alirai Ngunjiri.

Wakili huyo alisema Bw Maiyo amekuwa akijigamba hatambui maagizo ya mahakama na kuwahimiza wazazi wanachama wasihofu angali uongozini.

Jaji Thande aliamuru kesi isikizwe na Jaji Ong’udi ili awaadhibu Bw Maiyo na wenzake.

Alipoamuru Bw Maiyo ang’atuke uongozini wa NPA, Jaji Ong’udi alimwamuru asihutubie wanahabari ama kuhudhuria mikutano inayoitishwa na Wizara ya Elimu ama kujihusisha na utoaji wa misaada ya kimasomo kwa wanafunzi ama walimu wanaodhaminiwa na mashirika mbali mbali.

  • Tags

You can share this post!

Kibarua cha kusimamia serikali ya robo mkate

Aliyekuwa kiungo wa Nigeria, John Mikel Obi, astaafu soka...

T L