Habari Mseto

Agizo ardhi inayozozaniwa isiingiliwe hadi kesi isikizwe

February 11th, 2018 1 min read

Joseph Lenguris (kushoto) akitazama vijana wakiangusha lango la shamba linalozozaniwa eneo la Kikambala, Kaunti ya Kilifi jana. Bw Lenguris na mewe Bi Monika Behrmann anazoania umiliki wa ardhi hiyo na Bi Caroline Mwelu. Picha/ Kazungu Samuel

Na PHILIP MUYANGA

Kwa Muhtasari:

  • Shamba la mamilioni ya pesa eneo la Kikambala libaki lilivyo
  • Bi Caroline Mwelu Mwandiku anataka mahakama kumpa agizo la muda la kumzuia Bi Monika Herta Behrman kutojihusisha na shamba hilo
  • Kwa upande wake Bi Behrman katika ombi lake, anataka majina yake yatolewe katika kesi

MAHAKAMA ya Mazingira na Mashamba imeamuru kuwa shamba la thamani ya mamilioni ya pesa linalozozaniwa eneo la Kikambala libaki lilivyo kwa sasa.

Jaji Charles Yano, katika mahakama ya Mombasa, aliamua kuwa hali ilivyo katika shamba hilo imebaki vivyo hivyo hadi Aprili 16, wakati maombi mawili yaliyowekwa mahakamani na pande zinazozona yatasikizwa.

Katika ombi moja, Bi Caroline Mwelu Mwandiku anataka mahakama kumpatia agizo la muda la kumzuia Bi Monika Herta Behrman ambaye ni mmoja wa waliowasilisha maombi katika kesi kutojihusisha na shamba hilo liliko kaunti ya Kilifi.

Anataka pia kamanda wa polisi katika eneo la kilifi na maafisa wake waamuriwe kuhakikisha maagizo hayo ya mahakama yametimizwa.
Kulingana na ombi hilo, Bi Mwandiku anaishi na mwanawe wa kiume na wasichana wawili wadogo na ni mmiliki wa shamba hilo.

“Mlalamishi wa pili (Bi Behrman), bwanake na watu wanaofanya kazi kwa niaba yao, wametekeleza shughuli za uharibifu katika shamba hilo zikiwemo kuiba vitu vya thamani na vya kielektroniki,” ombi hilo lilisema.

Kwa upande wake Bi Behrman katika ombi lake, ambaye kulingana na karatasi Za kesi ni muweka kesi pamoja na Bi Mwandiku anataka majina yake yatolewe katika kesi.

Anataka pia kesi ambayo Bi Mwandiku aliwasilisha mahakamani kutupiliwa mbali.