TAHARIRI: Agizo kuhusu chanjo ya Covid-19 litaathiri uchumi nchini

TAHARIRI: Agizo kuhusu chanjo ya Covid-19 litaathiri uchumi nchini

Na MHARIRI

HATUA ya Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutoa agizo kila Mkenya awe amepokea chanjo ya corona ndipo aweze kupokea huduma muhimu, huenda likaleta madhara ya kiuchumi.

Ni miezi michache tu tangu Kenya ionyeshe dalili za kufufuka kiuchumi baada ya gonjwa la corona na kutikisa dunia nzima mwaka 2020.

Sababu kuu ambayo iliyomchochea waziri Kagwe kutoa agizo hili huenda ikawa ni kutokana na mapuuza ya wananchi kupokea chanjo ya Covid-19 na kugunduliwa kwa aina mpya ya corona nchini Afrika Kusini kwa jina Omicron, inayodaiwa kuwa hatari zaidi kuliko zile aina za awali.

Waziri Kagwe tayari ametangaza kwamba watakaokosa chanjo hii hawatapata huduma za serikali, uchukuzi na katika hoteli.

Hii ni kwa sababu tayari wamiliki wa hoteli wamefichua kwamba baada ya agizo hilo kutolewa, wageni wa kitaifa na kimataifa waliokuwa wamepanga kujivinjari kwenye mahoteli msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya, wameanza kufutilia mbali oda hizo.

Uchukuzi na utalii ni mojawapo ya sekta ambazo ziliathirika zaidi kutokana na maambukizi ya corona tangu mwaka 2020 kwa hivyo hatua inatosha kutishia kudidimiza tena licha ya kwamba zilikuwa zimeanza kufufuka.

Hii ina maana kwanza tayari wameanza kukadiria hasa watayopata kwa kipindi ambacho walikuwa wakikitegemea kiwapatie faida.

Wananchi wafaa kuelewa kuwa serikali haina nia mbaya mbali inalenga kulinda afya na maisha ya kila mmoja wao.

Pili, wafaa kujua kwamba suala la kiafya ni jukumu la kila mtu binafsi wala si serikali kuwashurutisha.

Wakenya wafaa kutii agizo hili na kukazana kupokea chanjo hio ili waweze kupata huduma hizo muhimu.

Isiwe kama inavyoshuhudiwa kila siku katika mikutano ya kisiasa ambapo wananchi hufurika bila kujali hata kidogo.

Itakuwa jambo la kutia moyo endapo Wakenya watawapuuza wanasiasa hawa wanaoendesha kampeni hizi kwa kuwa hakuna anayeshurutishwa kuhudhuria.

Hata hivyo, serikali inafaa kurahisisha huduma za kutoa chanjo ili Wakenya wengi waweze kupata dozi hizi kwa haraka kabla ya msimu ya sherehe unaobisha hodi kwa fujo sasa.

Aidha, serikali itilie maanani watakaoathirika hasa wafanyakazi, watalii na wamiliki wa biashara za utalii na uchukuzi ili ilegeze kamba Wakenya wengi wakipokea chanjo ya corona kuelekea Desemba.

Kuporormoka kwa sekta hii hakuathiri wadau pekee bali uchumi wa nchi nzima.

You can share this post!

Tabitha aidhinishwa na wazee kuwania wadhifa wa seneta

Messi aweka rekodi ya kushinda tuzo ya Ballon d’Or...

T L