NA MWANGI MUIRURI
MAAFISA wa usalama kaunti ya Murang’a bado hawajatii wito wa Naibu Rais Rigathi Gachagua wa kuhakikisha baa zinafuata sheria.
Alipozuru kaunti hiyo Alhamisi wiki jana, Bw Gachagua aliagiza maafisa wa usalama katika eneo la Mlima Kenya kuanza msako wa wafanyabiashara wanaouza pombe kinyume cha sheria.
“Hii tabia ya wamiliki wa baa kuvunja sheria ili kuwafanya vijana watumwa wa uraibu wa pombe lazima ikome. Msijali tu faida, muhimu ni hali ya kizazi cha baadaye na maafisa wote wanaotaka mema wanafaa kushughulikia suala hili,” alisema.
Badala ya kutii agizo hilo, maafisa wa idara tofauti za serikali ambao hutumia sekta ya pombe kujinufaisha walianza kurushiana lawama kuhusu hasa lilipo tatizo.
Baadhi ya wamiliki wa baa wamekuwa na ujasiri wa kukaidi huku mmoja wao mjini Maragua akiuliza mwandishi huyu:
“Unafikiri Gachagua anajua anachosema? Anafaa kuuliza aliyekuwa mbunge wa Naivasha John Mututho na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa nini walishindwa kukabiliana na sekta ya pombe.”
Mfanyabiashara huyo alimtaka Bw Gachagua “akusanye ushuru wake na kutuacha tuendelee na kazi zetu.”
Katika mji wa Murang’a na vitongoji vyake, magari rasmi ya kupiga doria ya polisi yangali yakizunguka jioni kukusanya ada za ulinzi kutoka kwa baa kama kawaida.
“Huwa tunalipa maafisa wa polisi Sh200 kila siku ili tuweze kukaidi sheria na kuhudumu kwa saa nyingi zaidi. Kile ambacho haturuhusiwi ni kuvunja sheria. Mradi tunafunga milango na wateja wetu kudumisha amani, tuko salama,” alisema mmiliki wa baa katika mji wa Kenol.
Uchunguzi kuanzia usiku wa Ijumaa, Jumamosi na Jumapili katika miji ya Murang’a, Maragua, Mabanda, Kenol, Kangari, Ngelelya, Kandara na Kiria-ini uligundua baa ambazo sio vilabu vya usiku zikihudumu baada ya usiku wa manane na kucheza muziki kwa sauti ya juu katika mitaa ya makazi.
Mwenyekiti wa Murang’a Youth Action Group Bw Waruinge Gitau anasema kwamba, kuwa na wawekezaji tofauti katika sekta hii kunafanya vigumu kukabiliana nayo na maafisa wengi wa polisi huamua ni salama kuchukua ada za ulinzi kuliko kujiweka katika hatari inayoweza kuwafanya wafutwe kazi.
Lakini maafisa wa usalama wanajitetea na kulaumu serikali ya kaunti kwa kutoa leseni za baa kinyume cha sheria.
“Tunataka serikali ya kaunti itusaidie kutekeleza sheria,” alisema Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Bw Ali Nuno.