Habari Mseto

Agizo magari Kaskazini yasisafiri bila ya polisi

February 21st, 2020 2 min read

JACOB WALTER, MERCY MWENDE na MANASE OTSIALO

SERIKALI imeamuru kwamba magari yote ya umma yanayotoka au kuelekea Kaskazini Mashariki yawe yakisindikizwa na polisi la sivyo, madereva watapokonywa leseni zao.

Kamishna wa eneo hilo, Bw Nick Ndalana, alisema uamuzi huo umefanywa kutokana na mashambulio ya kigaidi yaliyoongezeka.

Alisema pia madereva na wamiliki wa magari ambao hawatatii agizo hilo watashtakiwa.

Agizo hilo lilitokana na shambulio la basi katika eneo la Sarman mnamo Jumatano ambapo watu watatu waliuawa.

Akizungumza afisini mwake Marsabit, Bw Ndalana alisema basi lililoshambuliwa, lilikuwa linaelekea Nairobi ingawa lilipofika eneo la Sarman, washambuiaji takriban 11 waliokuwa kwenye pikipiki tatu walimwashiria dereva asimame.

Abiria watano walijehuriwa na kukimbizwa hospitalini huku wengine ambao walikuwa wamekimbilia vichakani wakati wa shambulio wakiokolewa na polisi.

Bw Ndalana alishangaa kwa nini gari hilo halikuwa na maafisa wa polisi wakati wa shambulio, kwani wakati lilipoondoka Mandera, kulikuwa na maafisa wa polisi kwenye basi.

Alielekeza Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) kuhakikisha agizo hilo limetekelezwa kikamilifu.

Bw Kilonzi Mwendwa, ambaye ni mmoja wa manusura wa shambulio la Mandera alisema walikutana na polisi mara mbili barabarani ambao waliwaambia usalama ulikuwa shwari.

Lakini takriban kilomita 70 kutoka mji wa Rhamu, wanaume walitokea barabarani wakiwa na bunduki katika pande mbili za barabara eneo la Sarman, Mandera Kaskazini.

“Dereva wetu hakusimamisha gari hata walipomsimamisha. Alijitahidi kuokoa maisha yetu kwani risasi zilikuwa zinafyatuliwa kutoka kila upande,” akaeleza.

Wakati dereva alipopunguza kasi baada ya kilomita moja hivi ili akague magurudumu yaliyoharibiwa na risasi, Bw Mwendwa anasema walianza kushambuliwa tena.

“Hapo ndipo watu walianza kukimbia. Nilifaulu kushuka gari kupitia dirishani nikajificha chini yake. Walikuwa wanaongea Kisomali lakini mmoja wao alitambua nilikuwa navuja damu akanipiga risasi tena,” akasema.

Msimamizi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mandera, Dkt Abdallah Hassan alisema manusura watatu waliolazwa katika hospitali hiyo hawamo hatarini.

Vile vile, serikali imepiga marufuku uendeshaji wa bodaboda kutoka Jumatano saa kumi na mbili jioni.

Marufuku hiyo itaathiri boda boda Kata ndogo ya Moyale, Mandera, Garissa, Wajir na kaunti za Lamu na Turkana.