Agizo picha za walaghai wa umeme zisichapishwe

Agizo picha za walaghai wa umeme zisichapishwe

Na BENSON MATHEKA

POLISI wameagizwa kutochapisha au kusambaza picha za washukiwa wanaodaiwa kujifanya wafanyakazi wa kampuni ya Kenya Power na kupokea pesa kutoka kwa raia wakidai wangewaunganishia stima.

Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Kibera Barbara Ojoo alitoa agizo hilo baada ya washukiwa kupitia wakili wao Samson Nyaberi kudai kwamba polisi walikiuka haki zao kwa kuwapiga picha bila idhini yao wakiwa seli za mahakama.

Bw Masese Elijah na Judith Kerubo walikamatwa wakiwa Nyamira Alhamisi wiki jana na kufikishwa jana katika mahakama ya Kibera jijini Nairobi kushtakiwa kwa kujifanya maafisa wa Kenya Power wakiwa na nia ya kulaghai.

Bw Nyaberi alishangaa ni kwa nini walisafirishwa kutoka Nyamira wanakoishi hadi Nairobi kushtakiwa na haki zao kukiukwa kwa kupigwa picha kinyume cha sheria.

“Hawakutenda uhalifu wowote hapa kortini. Kupigwa picha wakishika bango linalodai kwamba walitenda uhalifu ilhali wangali washukiwa ni kukiuka haki zao,” aliteta Bw Nyaberi.

Alilaumu maafisa wa polisi wanaolinda seli za mahakama kwa kuruhusu maafisa wa kuchunguza kesi kupiga picha wateja wake.

“Ninaomba mahakama iagize polisi wasitumie picha hizo kwa njia yoyote nchini Kenya, wasizichapishe na kuzisambaza kwa njia yoyote ile,” alisema.

Kwenye uamuzi wake, Bi Ojoo aliagiza polisi na kampuni ya Kenya Power kutotumia au kusambaza picha za washukiwa hadi wafike kortini kujibu madai ya wakili Nyaberi.

“Suala hili litashughulikiwa na hakimu atakayesikiliza kesi hii. Hata hivyo, ninatoa agizo picha hizo zisitumiwe kwa vyovyote vile,” alisema.

 

 

You can share this post!

Waliojaribu kuuzia polisi pembe huru kwa bondi ya Sh1m

Pasta atisha kushtaki mwenzake kudai anauza pombe

adminleo