Habari Mseto

Agizo wakili Nyakundi ajibu shtaka la kuua Agosti

July 27th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA kuu Ijumaa iliamuru wakili Assa Nyakundi afike kortini Agosti 12 kujibu shtaka la kumuua mwanawe, Joseph mnamo Machi 2019.

Na wakati huo huo, Jaji Jessie Lesiit aliamuru mawakili na kiongozi wa mashtaka Alexander Muteti wawasilishe maombi mengine yote baada ya mshtakiwa kujibu shtaka.

Jaji Lesiit alikuwa ameamuru kesi inayomkabili Bw Nyakundi itajwe mbele yake kutoa mwelekeo mpya baada ya majaji watatu kuamuru atoe maagizo jinsi itakavyosikizwa.

Majaji waliowaamuru mawakili Dkt John Khaminwa, Dunstan Omari na Mose Nyabenga wafike mbele ya Jaji Lesiit ni, Luka Kimaru, Ngenye Macharia na James Wakiaga.

Majaji hao watatu walikuwa wameombwa na mawakili wanaomwakilisha Bw Nyakundi waamue ikiwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) anakubalika kisheria kuwasilisha mashtaka mawili kuhusu mhasiriwa mmoja.

Katika ombi hilo , mawakili hao waliteta kwamba DPP, alimshtaki Nyakundi kwa kosa la kuua bila ya kukusudia.

Kabla ya kesi hiyo kusikilizwa katika mahakama ya Kiambu, DPP, aliwasilisha ombi la kuondoa shtaka hilo na “ kuwasilisha shtaka lingine la kuua akikusudia katika Mahakama kuu Nairobi.”

Mawakili hao wanasema katika ombi hilo kwamba DPP anatumia vibaya mamlaka yake kwa vile amemfungulia Nyakundi kesi mbili kuhusu mauaji ya mwanawe , Joseph.

“Hata kabla ya mahakama ya Kiambu kuamua ikiwa Nyakundi yuko na hatia ama hana , tayari DPP amewasilisha kesi nyingine,” Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Wakiaga.

Kutumia mamlaka vibaya

Wakili huyo alisema DPP anatumia mamlaka ya afisi yake vibaya ndipo akaomba mahakama kuu isitishe kusikilizwa kwa kesi hizo mbili ndipo mahakama iamue ikiwa kiongozi huyu wa mashtaka anatumia mamlaka yake vibaya.

Pia mahakama kuu ilikuwa inaombwa iamuru kesi ya Kiambu iendelee hadi tamati badala ya kesi “mbili kuhusu mtu mmoja kuendelea kwa wakati mmoja.”

Naibu wa DPP Bw Alexander Muteti anayeongoza kesi hiyo akisaidiwa na Bi Catherine Mwaniki, alikuwa ameeleza Jaji Lesiit kwamba atawasilisha ombi kesi hiyo ipelekwe kwa Jaji Mkuu David Maraga ateue jopo la majaji watatu kuamua masuala mbali mbali ya kesi hiyo.

Jaji Lesiit alitupilia mbali ombi hilo la DPP na kuamuru Nyakundi afike kortini kujibu mashtaka ya mauaji.

Agizo hilo liliwashtua mawakili wanaomwakilisha Nyakundi ambao walisema “ watafanya mashauri wajue jinsi kesi hiyo itakavyoendelea.”