Habari Mseto

Agizo waliomo vyuo vya ufundi wajiunge na shule za sekondari

February 17th, 2020 2 min read

Na PIUS MAUNDU

WANAFUNZI kadhaa waliojiunga na vyuo vya kiufundi Kaunti ya Makueni wamechanganyikiwa baada ya kupewa hadi mwisho wa wiki hii wajiunge na shule za upili.

Maafisa wa Elimu katika eneo hilo wanasema hatua hiyo imenuiwa kuhakikisha wanafunzi wote waliokamilisha shule za msingi wanajiunga na shule za upili.

Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti Ndogo ya Kibwezi, Bw Kennedy Machora, wiki iliyopita alivamia vyuo viwili katika eneo hilo akafurusha wanafunzi 70 waliokuwa wakifanya kozi mbalimbali za kiufundi.

Hatua hiyo ilishangaza wanafunzi, wazazi wao na maafisa wa serikali ya kaunti.

“Wanafunzi wote walio na umri usiozidi miaka 18 waliojiunga na vyuo anwai tangu mwaka wa 2017, wajiandae kujiunga na Kidato cha Kwanza,” akasema alipoenda katika Chuo cha Kiufundi cha Ngwata.

Alikuwa ameandamana na maafisa wa utawala wa eneo hilo Alhamisi.

Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti, Bw James Gachugi alisifu hatua hiyo akatoa wito kwa wakurugenzi wengine wa elimu katika kaunti zote ndogo kufuata mtindo huo wa Bw Machora.

Kulingana naye, wanataka wanafunzi 183 ambao walijiunga na vyuo vya kiufundi wakamilishe elimu ya sekondari kwanza.

“Tunashirikiana na wasimamizi wa vyuo vya kiufundi ili kutambua wanafunzi walio na umri wa chini ya miaka 18 ili tuwapeleke shule za upili kwa msingi wa agizo la serikali kuu,” akasema Bw Gachungi kwenye mahojiano jana.

Alidai kwamba wanafunzi hao hawana uwezo wa kutumia vifaa vinavyohitajika katika vyuo vya kiufundi.

Aliongeza kuwa, kwa kuwa hawajapokea mafunzo ya shule za upili, wanafunzi hao hawana uwezo wa kuelewa vyema yale watakayofunzwa katika vyuo anwai.

Msako uliofanywa haukufurahisha wanafunzi na wazazi. Baadhi ya wazazi wa wanafunzi walioathirika walisema waliamua kupeleka watoto wao katika vyuo vya kiufundi kwa vile hawana uwezo wa kugharamia elimu ya sekondari.

“Sasa elimu ya mtoto wangu imevurugwa,” akasema mmoja wa wazazi aliyeomba asitajwe jina.

Wakati mmoja, wasimamizi na maafisa wa mojawapo ya vyuo walilazimika kuingilia kati baada ya mmoja wa wanafunzi walioathirika kutishia kujitoa uhai na akaruhusiwa kuendelea hapo.