Agizo watumishi wakumbatie mavazi ya Kiafrika

Agizo watumishi wakumbatie mavazi ya Kiafrika

Na BENSON MATHEKA

WAFANYAKAZI wote wa umma sasa wanahitajika kuvalia mavazi ya Kiafrika na yaliyoshonewa humu nchini kila Ijumaa kulingana na agizo lililotolewa na Rais Uhuru Kenyatta, miaka miwili iliyopita.

Kwenye agizo lake la Oktoba 17, 2019, Rais Kenyatta aliagiza wafanyakazi wote wa umma, wawe wakivalia mavazi nadhifu yanayoakisi Ukenya wakiwa kazini kila Ijumaa na sherehe za kitaifaRais, alisema hatua hiyo itasaidia kufufua viwanda vya humu nchini.

Kwenye agizo hilo kupitia Afisi ya Mwanasheria Mkuu, serikali iliagiza watumishi wa umma kuhakikisha mavazi ya Kiafrika wanayovalia yatakuwa yameshonwa vizuri kufaa mazingara ya kazi zao.“Katika juhudi za kuafikia Ajenda Nne Kuu na hasa kupanua nguzo ya viwanda ya kutengeneza bidhaa bora na kubuni nafasi za ajira, ninaagiza kwamba wafanyakazi wote wa umma watakuwa kila Ijumaa wakivalia mavazi yaliyoshonewa Kenya,” ilisema ilani iliyotiwa saini na Wakili Mkuu wa Serikali, Bw Ken Ogeto.

Mnamo Jumatano, Wizara ya Utumishi wa Umma, iliagiza wakuu wa idara za wafanyakazi katika wizara na afisi zote za umma kuhakikisha agizo hilo linatakelezwa kikamilifu.Kwenye ilani, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Idara ya Serikali ya Utumishi wa Umma, Bi Margaret Wamoto, alisema kuvalia mavazi yaliyoshonewa Kenya kila Ijumaa kutakuwa sehemu ya mikataba ya utendakazi za watumishi wa umma.

“Kufuatia agizo la Rais kupitia ilani iliyosambazwa Oktoba 17 2019, watumishi wote wa umma, waliagizwa kuvaliwa mavazi ya Kikenya yaliyoshonewa nchini kila ijumaa. Hii imejumuishwa katika mikataba ya utendakazi kama mojawapo wa malengo ya mwaka wa kifedha wa 2020/ 2021,” Bi Wamoto alisema kwenye ilani kwa wakuu wote wa idara za wizara.

“Ilani hii basi, inanuiwa kukuomba uwakumbushe wafanyakazi walio chini yako kutimiza lengo hili,” alisema.Agizo hilo linaonyesha kuwa serikali imebuni njia za kuwalazimisha watumishi wote wa umma kuiga Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga ambao siku za hivi majuzi wamekuwa wakivalia mavazi ya kiafrika.

Hata hivyo, ikizingatiwa kwamba kila mtu ana haki ya kuvalia aina ya mavazi anayotaka, huenda agizo hilo likapata pingamizi kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.Lengo la serikali ni kuinua sekta ya viwanda vya nguo nchini.

Mnamo 2019, alipokuwa akifungua kiwanda cha nguo cha Rivatex mjini Eldoret, Rais Kenyatta alihimiza Wakenya kujivunia kuvalia mavazi yanayoshonewa humu nchini.“Ili serikali kuwa mfano, ninahimiza watumishi wote wa umma kuvalia angalau nguo moja iliyoshonewa Kenya kila Ijumaa,” alisema Rais Kenyatta wakati huo.

Mnamo Machi 2015, Wizara ya Mashauri ya Nchi za Kigeni, ilitangaza Ijumaa kuwa siku ya kuvalia mavazi ya Kikenya. Wizara hiyo ilisema kwamba Uafrika unapaswa kutumiwa kama chombo cha kidiplomasia.

Bi Wamoto alituma nakala ya ilani yake kwa wakuu wa idara zote za umma kuitekeleza kikamilifu kumaanisha kuwa watumishi watakaokosa kuvalia mavazi ya kiafrika kila Ijumaa huenda wakaadhibiwa wa kukosa kutimiza malengo ya kandarasi za utendakazi.

You can share this post!

Raila na Ruto wachuuza asali chungu

Kampuni yawafaa wakulima wa pilipili kwa kuunda bidhaa...

T L