Habari

Agnes Odhiambo ateuliwa mkuu wa NTSA

May 16th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WIKI hii wabunge wanawake walilalama kwamba jinsia hiyo inadhulumiwa baada ya Seneta wa Nakuru Susan Kihika kupokonywa wadhifa wa kiranja wa wengi katika seneti na kupewa mwanaume, Irungu Kang’ata, lakini pia Rais Uhuru Kenyatta amewatuza wanawake wawili kwa vyeo serikalini.

Amemteua aliyekuwa Msimamizi wa Bajeti (CoB) Agnes Odhiambo kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA).

Vilevile, Rais Kenyatta amemteua aliyekuwa Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) Profesa Mabel Imbuga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Kudhibiti Matumizi ya Pombe na Mihadarati (Nacada).

Teuzi hizo ni miongoni mwa nyingine nyingi ambazo Rais Kenyatta alifanya katika mashirika ya serikali na kuchapishwa katika toleo la Ijumaa la Gazeti rasmi la Serikali.

Bi Odhiambo na Profesa Imbuga watashikilia nyadhifa hizo kwa miaka mitatu, kuanzia Mei 13, 2020.

Mnamo Alhamisi wabunge 12 wanawake wakiongozwa na Mbunge wa Kandara Alice Wahome, walisema sio haki kwa Rais Kenyatta kumpa mwanamume cheo cha Bi Kihika.

“Mbona wanawake wanadhulumiwa ndani ya Jubilee ilhali walikuwa mstari wa mbele kuifanyia kampeni kufa na kupona katika chaguzi mbili zilizopita? Hata kama hawakutaka Seneta Kihika aendelea kuhudumu kwa wadhifa wa kiranja wa seneti nafasi hiyo ingepewa mwanamke mwingine lakini sio mwanamume,” akasema Bi Wahome ambaye ni kiongozi wa vuguvugu la ‘Inua Mama Jenga Jamii’.