Dondoo

Agonga mumewe kwa mwiko sababu ya mlo

February 25th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

WEBUYE MJINI

WAKAZI wa eneo hili, walibaki midomo wazi baada ya mwanadada kumlenga mumewe kwa mwiko wa kusonga sembe wakizozania kitoweo.

Kulingana na mdokezi, jamaa alitoka kazi ya mjengo na kupitia buchari na kununua kilo moja ya nyama akipanga kupigia mwili pole.

Baada ya upishi, kipusa alipakua chakula na kumpakulia polo vipande vichache vya nyama.

“Kwani nilinunua nyama kiasi gani ndio uniwekee vipande vitatu kwenye sahani?” polo alimuuliza mkewe.

Mama alimuangalia polo na kumtaka atosheke na alichowekewa mezani. “Unatakaje. Kula na uache maswali mengi,” alimkaripia polo.

Polo alimwangalia mkewe na kukataa kula. “Umenizoea sana. Kila wakati nikinunua nyama au samaki kwa hii nyumba, kazi yako ni kunijazia tu supu kwenye sahani,” polo alimfokea mkewe.

Hasira zilianza kumpanda mwanadada na kumjibu polo bila kujali lolote. “Wewe akili zako si sawa. Unabishana na mimi kwa sababu ya sufuria! Kesho nunua nyama uje ujipikie,” demu alimkaripia polo.

Inasemekana kwamba polo aliibua suala la ushirikiano baina yake na mkewe katika shughuli zote za jikoni lakini mkewe akapinga vikali.

“Kama umekosa kazi ya kufanya, nenda ukaajiriwe kuosha vyombo na kupika hotelini. Kazi ya jikoni ina mwenyewe,” demu aliwaka na kuelekea jikoni.

Aliporudi, mkononi alikuwa amebeba mwiko na sufuria iliyotumiwa kupika ugali.

Polo alipoona mambo si shwari, aliamua kukimbilia usalama wake huku akimweleza kipusa kuwa ataoa mke mwingine.

“Kwenda kabisa. Hakuna siku hata moja nitakuruhusu uingie jikoni,” kipusa alimueleza polo.