Michezo

Aguero asafirishwa Uhispania kwa matibabu

June 23rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MSHAMBULIAJI Sergio Aguero wa Manchester City sasa atasafirishwa hadi Uhispania kuangaliwa na mtaalamu wa majeraha ya magoti miongoni mwa wanasoka baada ya kocha Pep Guardiola kufichua kwamba huenda sogora huyo asiweze tena kucheza mechi yoyote msimu huu.

Aguero ambaye ni mzaliwa wa Argentina aliondolewa uwanjani kabla ya kukamilika kwa kipindi cha kwanza wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowakutanisha na Burnley uwanjani Etihad mnamo Juni 22, 2020.

Jeraha ambalo Aguero, 32, alipata katika mchuano huo ambao Man-City walisajili ushindi wa 5-0, lilikuwa zao la kukabiliwa visivyo na beki Ben Mee.

“Tathmini nilizofanyiwa zimebaini kwamba nilipata jeraba baya sana kwenye goti la kushoto. Hilo halitazima ari yangu kitaaluma, Nipania kupona hivi karibuni na kurejea uwanjani kwa matao ya juu na kishindo zaidi. Asanteni sana kwa jumbe za heri,” akaandika Aguero kwenye mtandao wake wa Twitter.

Katika mahojiano yake na wanahabari baada ya mechi, kocha Pep Guardiola alifichua kwamba Aguero amekuwa na tatizo la goti la kushoto kwa takriban mwezi mmoja uliopita ila hakuna yeyote aliwahi kutarajia kwamba angepatwa na yaliyompata dhidi ya Burnley kwa sababu alikuwa katika fomu nzuri mazoezini na hata kabla ya mechi.

“Amekuwa na jeraha kuanzia Mei 2020. Hata hivyo, maumivu hayo aliyokuwa akihisi kwenye goti la kushoto yamekuwa yakija na kupotea. Lakini jinsi alivyoondoka ugani inaibua hofu kwamba mambo si mazuri. Tuachie madaktari,” akasema Guardiola.

Nafasi ya Aguero katika mechi dhidi ya Burnley ilitwaliwa na Gabriel Jesus ambaye alichangia mabao yaliyofumwa wavuni na chipukizi Phil Foden, Riyad Mahrez na nahodha David Silva. Hadi waliposhuka dimbani kwa minajili ya mechi hiyo, Man-City walikuwa wamepiga Arsenal 3-0 katika gozi jingine la EPL.