Michezo

Agwanda atua jijini Lusaka kusajiliwa na Power Dynamos ya Ligi Kuu ya Zambia

September 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA msaidizi wa KCB, Godfrey Oduor, amethibitisha kwamba mshambuliaji wao Enock Agwanda amesafiri nchini Zambia kukamilisha uhamisho wake hadi kambini mwa Power Dynamos jijini Lusaka.

Mbali na Dynamos, huduma za Agwanda zimekuwa zikiwaniwa pia na klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Zambia (ZSL) zikiwemo Zanaco, Red Arrows na Green Buffaloes.

“Ameondoka humu nchini kwa pamoja na wakala wake kuelekea Zambia anakotarajiwa kupata hifadhi mpya kambini mwa Dynamos. Japo hakutoa maelezo ya kina kuhusu mkataba anaofukuzia katika kipute cha ZSL, alipata idhini ya klabu ya KCB kabla ya kufunga safari hiyo,” akasema Oduor.

Katika mahojiano yake na Taifa Leo mwanzoni mwa wiki hii, Agwanda alifichua kwamba alikuwa akiviziwa pia na Napsa Stars kabla ya kikosi hicho cha Zambia kumsajili fowadi Timothy Otieno wa Tusker kwa mkataba wa miaka miwili.

“Ningali na miezi sita zaidi kwenye mkataba wangu wa sasa na KCB. Hata hivyo, nimepokea ofa mbalimbali kutoka Zambia. Ninatafuta kikosi kitakachonipa jukwaa la kutamba zaidi ili nirejee katika timu ya taifa ya Harambee Stars itakayotegemewa na kocha Francis Kimanzi katika fainali za Kombe la Afrika (AFCON) za 2021,” akasema.

Katika kivumbi cha Ligi Kuu ya Kenya (KPL) msimu jana, Agwanda alifungia KCB jumla ya mabao 13 na kusaidia wanabenki hao kukamilisha kampeni katika nafasi ya tano.

Hadi aliposajiliwa na KCB mnamo Agosti 2019, Agwanda alikuwa pia amechezea SoNy Sugar (2011-12), Sofapaka (2013-15), Gor Mahia (2015-16), Bandari (2017) na Ushuru (2018).

Iwapo atafaulu kurasimisha uhamisho wake hadi Dynamos, Agwanda ataingia katima orodha ndefu ya Wakenya wanaonogesha soka ya kulipwa nchini Zambia wakiwemo Ian Otieno, Timothy Otieno, Jesse Were, David Owino, Musa Mohammed, Duke Abuya, Harun Shakava, John Makwatta, Ismail Dunga, Shaban Odhoji na Andrew Tololwa. Abuya na Shakava walisaidia Nkana FC kutawazwa mabingwa wa ZSL mnamo 2019-20.

Wakati uo huo, meneja wa timu ya KCB, Bramwel Simiyu, amethibitisha kwamba wanasoka Michael Mutinda na Baraka Badi wamerefusha kandarasi zao na wanabenki hao kwa kipindi cha mwaka mmoja zaidi.

Simiyu pia amefichua kwamba KCB wameagana na jumla ya wanasoka wanane hadi kufikia sasa na benchi ya kiufundi chini ya kocha Zedekiah ‘Zico’ Otieno inajitahidi kujaza mapengo yao.

Kati ya wanasoka wa haiba kubwa ambao wamekatiza uhusiano na KCB hivi majuzi ni Gabriel Mugabo, Bolton Omwenga, fowadi wa zamani wa Ulinzi Stars Stephen Waruru, beki wa zamani wa Gor Mahia na Kariobangi Sharks Pascal Ogweno na beki matata wa Harambee Stars Michael Kibwage.

Katika juhudi za kutafuta kizibo cha na nahodha Kibwage aliyesajiliwa na Sofapaka kwa mkataba wa miaka miwili, KCB kwa sasa wanamhemea beki matata wa Gor Mahia, Charles Momanyi.

“Kikosi kipo katika hatua za mwisho za kumsajili Momanyi na wanasoka wengine saba watakaotambulishwa rasmi kwa mashabiki kufikia mwisho wa wiki ijayo,” akasema Oduor.