Siasa

Ahadi juu ya ahadi

November 13th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA na VALENTINE OBARA

HOTUBA ya Rais Uhuru Kenyatta bungeni jana kuhusu hali ya taifa,ilisheheni msururu wa ahadi huku zile zilizotolewa hapo awali zikiwa bado hazijatimizwa.

Tangu 2017, Rais Kenyatta amekuwa akizingatia Ajenda Nne Kuu za maendeleo kama msingi wa kuhudumia wananchi hadi atakapostaafu kikatiba mnamo 2022.

Ajenda hizo zinahusu huduma bora za afya kwa wote (UHC), uzalishaji wa chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi wote, ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa Wakenya na ustawishaji sekta ya viwanda ili kutoa nafasi zaidi za ajira hasa kwa vijana.

Mpango wa UHC ambao majaribio yake yalizinduliwa mwaka uliopita, ulikumbwa na changamoto tele ukilenga kupunguzia umma gharama ya matibabu.

Rais Kenyatta jana alitaja changamoto hizo kama funzo, na kusema kuwa, kuendelea mbele, Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) itaboreshwa ili isaidie wananchi kugharamia matibabu yao.

Hivi sasa, NHIF inakashifiwa na wengi hasa kwa kukosa kugharamia matibabu ya virusi vya corona.

“Hakuna Mkenya anafaa kulazimika kuuza ardhi yake ili kupokea matibabu, au kulazimika kuchagua kati ya kununa dawa na kulisha watoto wake. Serikali inaendeleza mageuzi katika NHIF ili kuiboresha,” akasema Rais.

Alieleza matumaini kwamba, ushirikiano kati ya serikali kuu na za kaunti utafanikisha UHC.

Hata hivyo, Rais alionekana kusalimu amri kuhusu ahadi zake za awali, aliposema lengo la Ajenda Nne ni kuacha msingi thabiti wa maendeleo ifikapo 2022.

Hii ni tofauti na hotuba aliyotoa 2017, ambapo ahadi zilizo chini ya Ajenda hizo zilistahili kutekelezwa kabla aondoke mamlakani.

“Tulipounda Ajenda Nne tulifahamu fika kwamba, hazingekamilka kwa mkumbo mmoja. Mwishoni mwa 2022, tutakuwa tumeweka msingi thabiti kuhusu ruwaza hii,” akasema.

Katika sekta ya kilimo, wakulima wameahidiwa, kwa mara nyingine, kuwa mageuzi yatafanywa ili kuwasaidia.

Kwa miaka kadha sasa, wakulima hasa wa mahindi, miwa, majani chai na kahawa wamekuwa wakiahidiwa mageuzi ambayo yataongeza mapato yao.

Majopo yameundwa na ripoti zikatolewa, lakini malalamishi bado ni mengi kuhusu malipo duni na ukosefu wa usalama katika soko la mazao hayo.

“Mpango wa mageuzi unaendelea. Tumefanikiwa kufanya mageuzi katika mpango wa kusambaza pembejeo za kilimo,” akasema.

Sawa na katika hotuba zake nyingine, Rais alirejelea umuhimu wa vijana katika ujenzi wa taifa, huku akitaja mipango ambayo serikali inanuia kutumia kuinua hali ya maisha ya vijana.

Mojawapo ya mipango hiyo ni kuwawezesha kujisimamia kibiashara. Wakati huo huo, ahadi ya makao bora mijini pia ilirudiwa, ilhali utekelezaji wake umekumbwa na misukosuko.

Jana, Rais alisema shirika la kutoa mikopo ya kununua nyumba litasaidia kufanikisha ajenda hiyo, kando na ujenzi unaoendelezwa na serikali.

Katika sekta ya elimu, wananchi sasa wameahidiwa kwamba madarasa yasiyopungua 12,500 pamoja na majengo mengine muhimu ya shule yatajengwa katika miaka miwili ijayo.

“Ifikapo Desemba 1, 2020, Wizara ya Elimu na ile ya Ujenzi zitatoa mwongozo mpya kuhusu miundomsingi ya shule ili kupunguza gharama kwa kuzingatia mazingara ya maeneo tofauti nchini,” akasema Rais.

Licha ya hayo, Rais alieleza mafanikio kadha katika sekta ya usalama na miundomsingi.

Wabunge na maseneta waliohudhuria hotuba hiyo katika Bunge la Taifa walitoa hisia mseto. Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu, Bi Gladys Shollei alisema Rais “alipuuza kimakusudi sekta ya kilimo ambayo ni tegemeo la Wakenya”.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa na mwenzake wa Aldai, Cornelly Serem. Seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior aliunga mkono wito wa Rais kwa wabunge kwamba waelekeze sehemu kubwa ya fedha za CDF katika ujenzi wa miundo msingi shuleni. Hata hivyo, alisema wazazi watahitaji msaada kugharamia karo.

Kuhusu Mpango wa Maridhiano (BBI), Mbunge wa Garissa Mjini, Aden Duale alimkosoa Rais Kenyatta kwa kutotoa mwelekeo kamili kuhusu pingamizi zilizoibuliwa kuhusiana na yaliyomo kwenye ripoti hiyo.

Usalama uliimarishwa ndani na nje ya majengo ya bunge. Ni wabunge na maseneta 114 pekee waliruhusiwa ndani ya ukumbi kama sehemu ya hatua za kuzuia maambikizi ya Covid-19.