Habari Mseto

'Ahadi ya Sh53.5 bilioni kutoka kwa Uhuru haiambatani na sheria'

September 25th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

AHADI ya Rais Uhuru Kenyatta kwamba kaunti zitapewa nyongeza ya Sh53.5 bilioni kama mgao katika bajeti ya kitaifa katika mwaka ujao wa kifedha wa 2021/2022 huenda isitimizwe baada ya wabunge kuipinga.

Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Bajeti inasema ahadi hiyo ambayo inatarajiwa kufikisha mgao wa fedha kwa kaunti hadi Sh370 bilioni kutoka Sh316.5 bilioni katika mwaka huu wa kifedha wa 2020/2021 ni kinyume cha sheria.

Rais Kenyatta aliahidi nyongeza hiyo na hivyo kukomesha mvutano, miongoni mwa maseneta uliodumu kwa miezi mitatu, kuhusu mfumo bora wa ugavi wa fedha baina ya serikali 47 za kaunti.

Maseneta walikuwa wamefeli kukubaliana kuhusu suala hilo katika vikao 10, hadi Jumatano, Septemba 16, 2020, Rais alipokubana na uongozi wa seneti na kutoa ahadi ya nyongeza hiyo ya Sh53.5 bilioni.

Mkutano huo uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi, pia ulihudhuriwa na Kiongozi wa ODM Raila Odinga na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya.

Mvutano kuhusu mfumo huo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti ulisababishia kaunti changamoto za kifedha kiasi kwamba baadhi yazo zilishindwa kulipa mishahara ya wafanyakazi wao.

Hali hii ilisababisha Bw Oparanya kutoa agizo la kusitishwa kwa shughuli za utoaji huduma katika kaunti zote, zikiwemo zile za afya.

Ahadi ya kisiasa

Kamati hiyo ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge wa Kieni Kanini Kega imedai kuwa ahadi hiyo ya Rais Kenyatta ilikuwa ni “ya kisiasa wala haikutolewa kwa msingi wa utafiti wa kisayansi.”

Wanachama wa kamati hiyo walisema maseneta walitegemea ahadi ambayo huenda ikawa vigumu kutekelezwa.

Rais Kenyatta aliwafafanulia maseneta waziwazi pesa hizo zitatolewa tu iwapo hali ya uchumi itaimarika.

“Bunge la Kitaifa litaongozwa na uwepo wa rasilimali, masilahi ya kitaifa, kati ya masuala mengine wakati wa kufanya maamuzi kuhusu ugavi wa fedha kati ya Serikali Kuu na zile za kaunti,” kamati hiyo ikasema.

Kiongozi wa wachache John Mbadi ambaye ni mwanachama wa kamati hiyo alisema ni makossa kuandaa mswada wa ugavi wa fedha katika ngazi mbili za serikali kwa misingi ya ahadi, kwani Bunge linaweza kutenda kinyume.

“Hajaamua kuhusu Mswada wa Ugavi wa Fedha (DORB), wa mwaka wa kifedha wa 2021/2022 na tayari wameweka kiwango cha fedha wanachotaka kijumuishwe katika mswada huo. Ni kama kwamba serikali tayari imeamua na fedha hizo zinachukuliwa kana kwamba tayari zimetolewa. Hii sio kweli. Bunge linaweza kuamua vinginevyo,” akasema Bw Mbadi ambaye ni Mbunge wa Suba Kusini.

Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale alisema fedha hizo hazikuongezwa kisheria kwa sababu Mswada wa Ugavi wa Fedha baina ya Kaunti (CARA), 2020 hauwezi kusheheni kiasi tofauti cha fedha na mswada wa DORA, 2020 ambao ulitengea kaunti Sh316.5 bilioni.

“Kipengele cha 135 cha Katiba kinasema kuwa ikiwa Rais atafanya uamuzi, sharti uwe kwa maandishi na uwekwe ‘nembo’ rasmi. Fedha hizo za ziada hazitoahidiwa kwa mujibu wa sheria. Tunafaa kuzingatia mgao wa Sh316.5 bilioni ulioko katika mswada wa DORA, 2020,” Duale , ambaye ni kiongozi wa wengi wa zamani, akaeleza.