Dondoo

Ahamia kwa demu kuhepa mke kelele

October 22nd, 2019 1 min read

Na NICHOLAS CHERUIYOT

LITEIN, KERICHO

POLO wa hapa alizua mshangao alipofunganya virago kuhamia kwa kipusa mpango wake wa kando akilalama kuwa mkewe alikuwa akimkaripia vikali hadi akakosa raha.

Semasema za mtaa zaeleza kuwa jamaa na mkewe walikuwa na ndoa iliyojaa furaha hadi juzi ambapo kitumbua kiliingia mchanga baada ya jamaa kuonja asali ya nje.

“Polo alivutiwa na kidosho mmoja katika mji tofauti na alipomrushia ndoana akameza chambo. Kilichofuata kikawa ni jamaa kupagawishwa kwa mitindo ya kipekee ya mahaba na kisura huyo,” mdaku alieleza.

Mkewe jamaa alipong’amua ukweli wa mambo, alikosa raha na akajaribu mbinu zote kumnasua mumewe kutoka mikono ya kisura lakini ikashindikana.

Juzi, jamaa aliporudi kwake mkewe alimkemea vilivyo mbele ya majirani na kumwambia kuwa hatampa nafasi tena kuchovya asali yake.

“Wewe ni mtu bure sana! Badala ya kujiinua kiuchumi unajipeleka kwa kisura anayetamani tu hela zako. Hakuna uhusiano tena kati yangu na wewe, ni hii nyumba tu tutatumia pamoja. Hata haki yako ya ndoa hutawahi kuipata,” mrembo aliwaka.

Jamaa naye aliingia ndani ya nyumba akiwa ameaibika na mrembo akakereka mume kutojitetea au kuomba msamaha.

Muda mfupi baadaye, jamaa alitoka nje na kumuaga mkewe akidai alihamia mahali atapata raha.

“Naona ni heri nikuondokee ili nisife hapa kwa mawazo nawe ukae kwa utulivu,” jamaa alisema begi ya nguo mkononi.

Mkewe naye alimlilia asiende akiahidi kuwa hatampigia kelele tena na badala yake kutumia njia ya mashauriano kumaliza tofauti kati yao lakini jamaa akakaa ngumu.

Na Nicholas Cheruiyot