Michezo

Ahmed Musa mwanasoka bora wa Nigeria

April 2nd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

MSHAMBULIZI matata Ahmed Musa usiku wa Jumatatu, Machi 1 aliteuliwa mchezaji bora wa soka nchini Nigeria mwaka wa 2018.

Musa, 26 aling’aa sana kwenye Makala ya Kombe la Dunia ya mwaka wa 2018 yaliyoandaliwa nchini  Urusi na pia mechi nyingine alizowajibikia wakati taifa hilo lilipokuwa likishiriki mechi za kuwania kufuzu kushiriki Kombe hilo.

Kwenye kipute cha Kombe la Dunia, fowadi huyo wa klabu ya Al-Nassr, Dubai alifungia Nigeria inayonolewa na Gernot Rohr mabao mawili muhimu katika mechi za makundi.

Mchezaji huyo wa zamani wa Leicester City inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza(EPL)  pia aliifungia Super Eagles mabao muhimu  wakati wa mechi za kimataifa tangu mwaka wa 2013.

 Hata hivyo, fowadi wa Super Eagles  Odion Ighalo na winga wa Arsenal  Alex Iwobi walimpa upinzani mkali Musa kwenye uwaniaji wa tuzo hiyo lakini hatimaye alitangazwa mshindi kwenye sherehe ya kufana iliyohudhiriwa na wanasoka wa zamani pamoja na maafisa wa serikali katika mkahawa moja mjini Lagos.

Mshambulizi huyo pia alitwaa tuzo ya mfungaji aliyefunga bao bora  tena kwa ustadi mkubwa  mwaka jana. Musa alilifunga bao hilo wakati wa mechi dhidi ya Jamuhuri ya Iceland wakati wa Kombe la Dunia.

Wakati uo huo Samuel Chukwueze anayesakatia Villarreal ya Uhispania  alitwaa tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa 2018 baada ya kuwapiku Henry Onyekuru wa Galatasaray na Victor Osimhen wa Sporting  Charleroi.