Kimataifa

Aiba gari dakika chache baada ya kuwachiliwa kutoka jela

October 25th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

TOPEKA, KANSAS

MWANAMUME kutoka Kansas alikamatwa punde tu baada ya kuachiliwa kutoka gerezani, kwa kuiba gari lililokuwa limeegeshwa katika eneo la maegesho la gereza hilo.

Kulingana na mashirika ya habari ya taifa hilo, Bw Kevin Jones wa miaka 33 aliiba gari hilo alipowachiliwa huru kutoka jela ya Kansas, Jumapili asubuhi.

Camera za siri katika gereza hilo zilimwonyesha Bw Jones akivunja na kuingia ndani ya gari hilo kisha kuliendesha, lakini akapatikana na mwenye gari eneo jirani na gereza hilo.

Mmiliki wa gari pamoja na baadhi ya majirani walimzuilia mwanaume huyo hadi polisi walipofika na kumkamata. Alirudishwa katika jela hiyo na kufunguliwa mashtaka ya wizi wa gari na kuvunja mali kwa njia haramu.

Hata hivyo, Bw Jones siye mtu wa kwanza kuiba gari katika eneo la maegesho la jela hiyo baada ya kuwachiliwa, kwani mwaka uliopita, mvulana wa miaka 18 naye aliruka ukuta kuelekea eneo wanapoegesha magari wafanyakazi wa jela hiyo na kuvunja magari kadha lakini akakamatwa pia na kufunguliwa mashtaka mapya.