Dondoo

Aiba mahindi ya mke apate hela za kubet

April 15th, 2019 1 min read

Na DENNIS SINYO

MBAI FARM, KITALE

KALAMENI wa hapa alijipata kona mbaya alipofumaniwa akiiba mahindi ya mkewe ili ayauze apate pesa za kucheza kamari.? Inasemekana jamaa alianza kubet bila kujua athari zake hadi akawa mtumwa wa tabia hiyo.

Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa na mazoea ya kuiba pesa za mkewe ili kushiriki kamari lakini hakufanikiwa kushinda hata siku moja.

Licha ya kuonywa aache tabia hiyo jamaa huyo hakuacha kushiriki kamari. Siku ya kisanga, jamaa alifumaniwa na mkewe akiiba mahindi ili kuyauza.

Inasemekana tayari alikuwa amepata mteja aliyekuwa akisubiri mahindi hayo ampe pesa. Mkewe alijawa na hasira na akamfokea kwa kupita mipaka.

“Umeibia watu wengi kijijini na sasa umeamua kuiba hata kwa nyumba yako mwenyewe? Jamani nani alikuroga wewe mwanaume?”aliuliza mkewe huku akilia.

Jamaa alipata aibu ya mwaka na akaamua kuyarejesha mahindi hayo kwenye gunia. Mkewe alidai kwamba alikuwa amechoshwa na sarakasi za mumewe akisema ndoa hiyo ilikuwa imekosa ladha.

”Unaishi na mume ambaye unamsaidia kwa kila kitu na mwishowe anakuibia tena,” alilia mke wa jamaa.

Mama huyo alishangaa kwa nini mumewe alikuwa amejiingiza kwenye uraibu wa kamari akijua kwamba hakuwa na pesa.

”Tangu uanze kucheza, ni lini umesema umeshinda milioni? Watu wanajiua kwa kupoteza hela zao na wewe bado unazidi kucheza bila kuwa makini,” aliongezea mkewe.

Mama huyo alitisha kumuacha jamaa akisema ndoa yao haikuwa na mwelekeo. Alidai tangu waoane, hawakuwa wamepiga hatua yoyote kutokana na visanga vya jamaa.

Mumewe hakusema jambo, alinyamaza na kutoka nje akiwa ameinamisha kichwa.