Habari Mseto

Aibu kizimbani mwanamume kubaka nyanyake wa miaka 90

June 18th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME kutoka Kaunti ya Kakamega Jumanne alishtakiwa kwa kumbaka nyanyake wa miaka 90.

Protus Amusibwe alishtakiwa kuwa mnamo Juni 8, 2019 alitoboa shimo katika nyumba ya nyanyake ya matope, katika kijiji cha Ilenyi, eneo la Kakamega Mashariki, kisha akaingia na kumbaka.

Korti ilielezwa kuwa mshukiwa alimvamia nyanyake wakati kulikuwa kukinyesha na kuwa mayowe ya ajuza huyo hayangesikika, huku pia akiwa alikuwa akimziba mdomo alipokuwa akimtendea unyama huo.

Mshukiwa alisemekana kumbaka hadi asubuhi, kisha akatoroka.

Alikamatwa siku tatu baadaye, wakati umma ulikuwa ukitaka kumuua kwa kumpiga mawe, lakini polisi wakafika na kumuokoa.

Jumanne, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi wa Kakamega Erick Malesi, ambapo alipinga kuwa alimbaka ajuza huyo.

Kesi hiyo itatajwa Julai 5 na kuanza kusikizwa Agosti 8.