Habari

Aibu kwa viongozi wa Laikipia wanafunzi kutumia mawe kama madawati

March 22nd, 2018 1 min read

NA PETER MBURU

WAKENYA wameshuhudia baraka na maafa mengi kwa watu, mifugo na maeneo mbalimbali nchini katika msimu wa mvua mwezi Machi.

Kwa watoto wanaosomea katika Shule ya Msingi ya Kianjogu iliyoko Laikipia Magharibi, hata hivyo, hali si hali tena kutokana na mazingira mabovu, ya aibu na hatari kwa afya ya watoto wa shule hiyo.

Hii ni kutokana na madarasa ya shule hiyo kukosa mahitaji yoyote ya kimsingi kuwasitiri watoto kutokana na kijibaridi na mvua wakati kunaponyesha.

Kunaponyesha katika eneo la Laikipia, wanafunzi katika Shule ya Msingi ya Kianjogu hawana pa kujikinga kijibaridi huku madarasa yakijaaa maji wasijue pa kusimama. Badala ya madawati, wanafunzi hawa hutumia mawe na mbao. Hali kama hii yaweza kuwasababishia magonjwa kama Bilharzia. Picha/ Peter Mburu

Madarasa ya shule hiyo hayana kuta wala ndani hakuna madawati, ila watoto wanatumia mawe na magogo ya miti kuandikia huku wakikalia mawe.

Vilevile, wakati kunaponyesha, madarasa hufurika maji machafu hali inayowasukumia watoto kusomea madarasa yasiyo na hamu yoyote ya kukidhi kiu ya elimu ya watoto.

Walimu wa shule hiyo pia wanavumilia hali duni kwani afisi zao ni picha nyingine ya fedheha, kwa kukosa miundomsingi ya kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

Hali ilivyo katika shule hii. Wanafunzi hufundishwa wakiwa wamekalia mawe huku wakitumia mbao kama dawati. Picha/ Peter Mburu

Ni mazingira ya aibu kwa wazazi, wanao, walimu na hata viongozi wa eneo hilo na picha zake zinaashiria ugumu apitiao mtoto kutoka kaunti ya Laikipia ili kuafikia ndoto yake kielimu.

Taifa Leo ilipotembelea shule hiyo Alhamisi ilidhibitisha hali mbovu ya miundomsingi yake, ila hakukuwa na wanafunzi wala walimu kwani walikuwa michezoni katika shule nyingine.

Darasa hili halina madawati wala ubao wa kufundishia. Wanafunzi huweka vitabu juu ya fomu ambapo vinaweza kuanguka kwa maji kunaponyesha. Picha/ Peter Mburu

Viongozi nao wakiongozwa na mbunge wa Laikipia Magharibi Patrick Mariru, bali na kutelekeza majukumu yao, wamejaribu kujiepusha na aibu hiyo, akisema shule hiyo haiko katika eneobunge lake.

“Hatukatai kuwa mazingira ya shule ya Kianjogu si ya kuridhisha, lakini  picha zinazosambaa ni za shule nyingine wala si ya Kianjogu,” akasema msemaji wa mbunge huyo.

Hali hiyo ya viongozi kufumbia macho masuala muhimu katika meneo yao inatoa ishara ya kutowajali wakazi waliowachagua, uzembe, ukiukaji wa haki za watoto na ubinafsi wa hali ya juu kwani inaanika jinsi pesa za Hazina ya Maeneobunge (CDF) zinatumika vibaya .