Habari Mseto

Aibu machifu kuwalinda wanajisi

July 23rd, 2018 1 min read

Na BRUHAN MAKONG

MWAKILISHI wa Kike wa Kaunti ya Wajir Fatuma Gedi amewaonya machifu dhidi ya kuwalinda wanajisi wa wanafunzi.

Bi Gedi alisema machifu hao wanasitiri washukiwa kwa kuwapatanisha na familia za waathiriwa na kuwatoza faini nje ya mahakama.

Mbunge huyo aliyekuwa akizungumza katika shule ya msingi ya Griftu alisema washukiwa wa ubakaji wa wasichana ni sharti wafikishwe mahakamani.

Alisema machifu hawaruhusiwi kisheria kushughulikia kesi zinazohusiana na dhuluma za kimapenzi dhidi ya wasichana.

Badala yake aliwataka machifu kushirikiana na polisi kuwanasa wahalifu hao wanaonajisi wanafunzi wa kike.

Idadi kubwa ya wasichana hulazimika kuacha shule baada ya kupachikwa mimba katika kaunti hiyo.

Machifu wamekuwa wakikashifiwa kwa kutumia utaratibu wa kitamaduni unaofahamika kama ‘maslaha’ kusuluhisha kesi zinazohusiana na unajisi wa watoto.

“Machifu wanafaa kuhakikisha kwamba washukiwa wanashtakiwa mahakamani. Utamaduni wa ‘maslaha’ ambapo washukiwa wanatozwa faini kidogo na baadaye kuachiliwa huru, haufai,’ akasema.

Wajir ni miongoni mwa kaunti zilizo na visa vingi vya dhuluma za kimapenzi dhidi ya watoto wa kike.

Bi Gedi aliahidi kuendelea kutoa sodo kwa wanafunzi kuwazuia kutoenda shuleni wakati wa hedhi.

“Hakuna msichana ataacha kwenda shule kwa sababu ya hedhi. Afisi yangu itashirikiana na wahisani wengineo kuhakikisha kuwa kila msichana ananufaika kwa sodo,” akasema.