Habari Mseto

Aibu msafishaji kuiba kompyuta ya NMG

March 6th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSAFISHAJI katika jengo la Nation Centre alishtakiwa Jumatano kwa kuiba tarakilishi yenye thamani ya Sh80,000.

Bw Paul Otieno Omolo alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot. katika mahakama ya Nairobi.

Alikana aliiba tarakilishi hiyo kutoka orofa ya nne katika jengo la Nation Centre, ambayo ni mali ya kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG).

Bw Omolo mwenye umri wa miaka 35, alidaiwa aliiba tarakilishi hiyo mnamo Feburuari 25 mwaka huu.

Aliomba aachiliwe kwa dhamana akisema tangu alipotiwa nguvuni amekuwa mgonjwa.

Akarai, “Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana. Nimekuwa mgonjwa na naomba nipewe dhamana isiyo ya kiwango cha juu. Nilikuwa nje kwa dhamana ya polisi ya Sh35,000. Naomba niachiliwe kwa kiwango sawa na hicho.”

Mahakama ilimwachilia mfanyakazi huyo wa kampuni ya Foresight Cleaning kwa dhamana ya pesa taslimu za kiwango alichoomba ama bondi ya Sh200,000.

Kesi yake itatajwa baada ya wiki mbili.