Michezo

Aibu ya mwaka Asante Kotoko ya Ghana kuiba taulo za hoteli ya Nairobi

December 17th, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

ILIKUWA aibu ya mwaka kwa kikosi cha Asante Kotoko kumulikwa kwa kuiba taulo za uso katika hoteli moja jijini Nairobi  baada ya mechi yao ya kuwania ubingwa wa Kombe la Mashirikisho (CAF) dhidi ya Kariobangi Sharks Jumamosi Disemba 15 kwenye uga wa MISC Kasarani.

Wachezaji wa timu hiyo kutoka Ghana wanadaiwa kutoka hotelini humo na taulo hizo kati ya bidhaa nyingine, tukio ambalo Afisa Mkuu Mtendaji wa klabu George Amoako ametaja kama halingefaa kutokea.

“Zilikuwa tu taulo za uso. Ni tukio tunalolisikitikia ila tutalitatua vizuri,” akasema Amoako.

Hata hivyo usimamizi wa hoteli hiyo ulikataa kuzungumzia suala hilo ulipofikiwa na wanahabari.

Sare tasa iliyosajiliwa Jumamosi na timu hizo mbili inaiweka Asante Kotoko katika hatua nzuri ya kufuzu iwapo itaifunga Kariobangi Sharks na pia kujiepusha na sare ya idadi yoyote ya mabao.

Mechi ya marudiano  itagaragazwa katika uwanja Baba Yaro Sports Stadium mjini Kumasi Disemba 22.

Lakini kisa hicho cha wizi kitasalia kwa akili za Kariobangi Sharks, ambao lazima wajikakamue kuwabandua.