Habari

Aibu ya wakazi Nyeri kugeuza mashamba ya majani chai kuwa danguro

August 24th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

WAKAZI wa Nyeri wameshangaza ulimwengu tena, baada ya kubainika kuwa wamegeuza mashamba ya majani chai kuwa sehemu za kujiburudisha kimapenzi, kutokana na uhaba wa ‘lojingi’ na ukosefu wa pesa miongoni mwa vijana.

Tabia hii inayohusisha vijana kwa wazee, hata wengine wakiwa wanafunzi sasa imetia doa maadili ya jamii ya kaunti hiyo, haswa katika maeneo yanayokuzwa majani chai, ambayo yamezongwa na visa hivyo.

Mashamba ya mmea huo yanasemekana kutapakaa mipira ya kondomu na nguo za ndani, ishara kuwa ‘maajabu’ mengi hutendeka humo ndani.

Baadhi ya wakazi walieleza Taifa Leo kuwa mashamba hayo yamekuwa chaguo lao bora kujipa burudani hiyo ya usiri, kwa kuwa hawalipi chochote, ilhali hakuna usumbufupu wajiburudishapo.

“Kwa kuwa hakuna nyumba za kukodi kujiburudisha hapa karibu, tunaamua kwenda ndani ya mashamba haya. Ni gharama kwenda lojing’i kwani mwanzo itatubidi kwenda hadi nyeri Mjini,” akasema kijana mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Lakini kuzidi tabia hiyo kumeibua hofu hata miongoni mwa maafisa wa afya kuwa kunachafua mazingira na kuacha vifaa vyenye uchafu mahali watoto wanaweza kuvifikia na kupata maradhi.

Baadhi ya wanaojihusisha na tabia hiyo ni vijana ambao wanaishi pamoja na wazazi wao na ambao bado hawajaruhusiwa kujihusisha na masuala ya mapenzi, wengi wao wakipotezea ubikira ndani ya mashamba hayo.

Vilevile, uozo zaidi umeripotiwa pale vijana wa umri mdogo hujihusisha na wazee katika mapenzi kwenye mashamba hayo, huku wazazi wengi wakisalia gizani kuhusu wanachofanya wanao.

“Hii ni kweli kabisa, kwa kweli Tetu hakuna kituo cha mafuta, benki wala danguro pamoja na vifaa vingine vya kimsingi. Hali hii imechangia kuongezeka kwa visa hivi,” akasema James Muringo, mkazi.

Aliongeza kuwa mara nyingi hata wanandoa wanapotaka kuonja asali ya pembeni ama watu walioishiwa kifedha kujiburudisha, chaguo lao  mashamba ya majani chai.