Habari Mseto

Aililia mahakama baada ya kutisha kumuua bawabu

March 22nd, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Alhamisi kwa kutisha kumuua mlinzi katika mtaa wa Kileleshwa kaunti ya Nairobi siku tano zilizopita.

Bw Kevin Obia alikanusha mashtaka mawili ya kutisha kumuua bawabu Yohana Imbwaka na kutoa bastola mahala pa umma.

Alipofikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bw Peter Ooko, Bw Obia alikanusha mashtaka mawili dhidi yake na kuomba aachiliwe kwa dhamana.

“Naomba hii mahakama iniachilie kwa dhamana,” Bw Obia alimsihi hakimu.

Akaongeza, “Nilikuwa nimeachiliwa kwa dhamana ya Polisi ya Sh10,000. Naomba korti iniachilie kwa kiasi sawa na hicho nilichokuw3a nimepewa na Polisi.”

Kiongozi wa mashtaka Bi Celestine Oluoch hakupinga ombi la mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Hakimu alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh500,000 na kuorodhesha kesi isikizwe mnamo Aprili 30,2019.

Ikiwa mshtakiwa atashindwa kulipa dhamana hiyo ya pesa tasilimu mshtakiwa aliagizwa awasilishe dhamana ya Sh1milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.

“ Naamuru upande wa mashataka ukukabidhi nakala za mashahidi  katika muda wa wiki mbili. Kesi hii itatajwa Aprili 4, 2019 upande wa mashtaka uthibitishe ikiwa umekupa nakala za mashahidi,” aliamuru hakimu.