Kimataifa

Aina mpya ya corona hatari zaidi yapatikana Uingereza

December 22nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

UINGEREZA ‘imetengwa’ na mataifa ya Umoja wa Ulaya (EU) baada ya wanasayansi nchini humo kugundua aina mpya ya virusi vya corona vinavyoaminika kuwa hatari zaidi.

Mataifa ya EU; Ufaransa, Ujerumani, Italia, Denmark, Uswisi, Ireland, Austria, Ureno, Sweden na Ubelgiji tayari yamepiga marufuku ndege kutoka nchini Uingereza.

Bulgaria pia imezuia safari za ndege kati ya nchi hiyo na Uingereza. Serikali ya Bulgaria ilisema kuwa marufuku hiyo itaisha Januari 31, mwaka ujao. Uturuki na Uswisi pia zimesitisha safari za ndege kutoka Uingereza.

Canada imepiga marufuku ndege za abiria kutoka Uingereza kwa saa 72.Ufaransa ilitangaza Jumapili hatua yake ya kusitisha safari zote kati ya nchi hiyo na Uingereza kwa muda wa saa 48.

Mataifa mengine ambayo yamepiga marufuku ndege kutoka Uingereza ni Hong Kong, Israeli, Iran, Croatia, Argentina, El Salvador, Chile, Morocco na Kuwait.

Saudi Arabia imesitisha safari zote za kimataifa kwa kipindi cha wiki moja kufuatia kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya corona nchini humo.

Kulingana na wanasayansi, virusi vipya vya corona vilivyogunduliwa vinaenea kwa kasi kusini mwa Uingereza.Wataalamu wanasema kuwa virusi hivyo vinajibadilisha mara kwa mara.

Wataalamu sasa wanahofia kuwa chanjo inayoendelea kutolewa kuzuia virusi vya corona nchini humo huenda ikakosa kufanya kazi.

Waziri wa Afya wa Uingereza Matt Hancock alisema kuwa virusi hivyo vipya vya corona vinasambaa kwa kasi ya juu na huenda serikali ikalemewa.Kiongozi wa chama cha Labour, Sir Keir Starmer, jana alimtaka Waziri Mkuu Boris Johnson kuhutubia taifa kuhusu aina hiyo mpya ya virusi vya corona.

‘Taarifa kuhusu virusi vya corona ndani ya saa 24 zilizopita zinashtua. Idadi ya visa imeongezeka maradufu ndani ya wiki moja,” akasema.Aina hiyo mpya ya virusi vya corona pia imegunduliwa nchini Afrika Kusini.

Wataalamu nchini Afrika Kusini, hata hivyo, wanasema virusi walivyogundua ni tofauti na vile vilivyopatikana Uingereza.Wataalamu wa Afrika Kusini wanasema kuwa wangali wanafanya utafiti zaidi ili kubaini madhara ya virusi hivyo vipya vya corona.

Aina mpya ya virusi vya corona iligunduliwa kwa mara ya kwanza mkoani Eastern Cape lakini sasa vimesambaa katika mikoa ya Western Cape na KwaZulu-Natal.

Wanasayansi nchini Afrika Kusini wiki iliyopita walisema kuwa aina hiyo ya virusi vya corona vimekuwa vikilemea vijana zaidi.Serikali wiki iliyopita ilitangaza vikwazo zaidi ili kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona katika msimu huu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Miongoni mwa mikakati ni kufungwa kwa baadhi ya fukwe za bahari ambazo huwa na msongamano mkubwa wa watu wakati wa sherehe.