Habari

Aina tano za mizigo ambayo mja anafaa kuepuka maishani

July 9th, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

BINGWA wa kihistoria, Winston Churchill, akikaribia kuaga dunia alikuwa na masikitiko.

“Nikiangalia mkondo wa maisha ya uhai wangu hadi sasa, naona masikitiko mengi na kunifanya nikumbuke wosia wa mwingine akifariki aliyesema hayo masikitiko, mengi ya hayo hata hayakuweko.”

Ni maneno yanayoweza yakakukanganya hasa ikiwa fasihi sio fani yako pendeka, lakini kwa upole na urahisi Churchill anakuhimiza usiwe wa kuzingatia sana masikitiko uliyo nayo katika maisha.

Kwa upana, kuna ile mizigo ya mawazo ambayo watu hujiwekelea katika mabega yao, zingatia neno ‘hujiwekelea’, na kisha wanashinda na wanakesha wakinuna kuwa maisha ni magumu.

Kasisi Lawrence Chege anashauri waja kuepuka baadhi ya mizigo maishani.

“Wewe weka hiyo mizigo chini, jipe raha, kuwa mkakamavu na ujue wengi wako katika hali mbaya afadhali hiyo yako. Pengine hujui kwa sababu wameamua kupuuza hayo mahangaiko ili kujipa raha,” anasema Kasisi Chege.

Anakukumbusha kuwa Biblia imejaa maneno ya utulivu na kukupa hifadhi hasa katika Matayo 11:28-30 ambapo unaagizwa “kuja kwangu enyi nyote mlio na mizigo mizito na nitawapa pumziko…”

Kati ya hiyo mizigo mizito unayoombwa usiwe wa kubebana nayo katika maisha yako ni pamoja na taharuki.

Mhenga Ten Boom alinena kuwa taharuki au uoga katika maisha huzidisha kesho yako kuwa ngumu kuiishi.

Alisema kuwa hali hiyo ya uoga au taharuki hupunguza uwezo wako wa kila siku wa kumenyana na mawimbi ya maisha na hivyo basi ni lazima ujiepushane na kuwa mtumwa wa uoga au taharuki.

Katika kitabu chake Affluenza, mwanasaikolojia Oliver James anasema kuwa wengi hujitwika hali ya mahangaiko kupitia kukubali maisha ya uoga na taharuki; hivyo basi kujipa shinikizo zisizosaidia maisha yako na hatimaye unajipata ukiugua kisukari, misukumo ya damu na hata kurukwa na akili.

Anakwambia usiwe wa kuzingatia mabaya kutokea katika maisha yako, yakija sasije isiwe ni kitu, bora tu ujipe raha na utulivu wa maisha yako kwa kuwa Mungu ako usukani.

Hisia za kufeli

Mahangaiko mengine ya kimaisha na ambayo ni mzigo ni hisia za kufeli.

 

 

Kasisi Lawrence Chege wa Kanisa la PCEA, Murang’a. Picha/ Mwangi Muiruri

Hii inaweza kuwa kufeli mtu ambaye ni mwandani wako na unaishia kumsaliti au ile hali ya kuhisi kuwa hujafanikiwa katika maisha yako hivyo basi kujiorodhesha kama wale wamefeli kuafikia vigezo vya hadhi kimaisha.

Hali hizo mbili bado zinasemwa kuwa ni mzigo wa kimaisha ambao hautakupa raha na unafaa kujiepusha nazo.

Mzigo mwingine wa kimaisha ambao ni sharti uangushe kutoka mabegani mwako ni wa kuhujumu haki.

Ikiwa wewe ni msomi wa Biblia, utaelewa kuwa Yesu Kristo alikumbana na usaliti huu wa haki ambapo alihukumiwa kusulubiwa licha ya kuwa waliokuwa wanastahili kuadhibiwa walikuwa ni wezi wa enzi hiyo wakiongozwa na Baranaba.

Hata hivyo, kwa kuwa wewe sio Yesu na haujawekwa katika hukumu ya kusalitiwa haki, unazingatiwa uishi maisha ya haki kwa wote na katika hali zote, uwe wa kuimarisha haki kunawili na kukita mizizi katika jamii.

Mzigo mwingine mbaya unaohimizwa usiwe wa kujiwtika mabegani mwako ni ule wa dhambi.

Huu ni mzigo ambao unaambiwa ulibebewa na Yesu katika safari yake ya msalaba na kamwe huna kisingizio cha kutekwa nyara na dhambi kiasi cha kuishi maisha ya mahangaiko ukingoja adhabu ya Mungu ambayo itazingatia haki katika hali zote.

Na katika maisha yako, Kasisi Chege anakuhimiza usiwe wa kuishi maisha ya kulemewa na majuto kwa kuwa yaliyotendeka yalitendeka na hayana cha pole.

Anasema kuwa ukishajipata katika hali ya kukupa majuto, sahau yametendeka na uombe Mungu akuondolee huo mzigo katika maisha yako.

Anasema kuwa kwa kuwa ukiwa na maono ya kesho yako unafaa kuyaona maisha ambayo ni ya utulivu, ukisahau matukio yanayokupa hisia za majuto, utayaafikia.

Katika hali zote, cha kusisitiza, huu ukiwa ni ufupisho wa haya yote umeyasoma hapa, ni kuwa uzingatie kuishi maisha yasiyo na hali za uoga, kuhisi umefeli hali yoyote, majuto, dhambi na usaliti kwa haki.

Hayo ndiyo maisha ya kuishi na ambayo yataishia kukupa utulivu.