Makala

Aina tofauti za kumbikumbi kitoweo cha jamii ya Abaluhya

May 5th, 2019 3 min read

Na GEOFFREY ANENE

KWA miaka mingi, mlo wa kumbikumbi umekuwa ukitawala meza za wakazi wa Mkoa wa Magharibi hasa za jamii ya Waluhya na haikuwa tofauti mwezi Aprili Taifa Leo Dijitali ilipozuru maeneo hayo na kung’amua mengi kuhusu mlo huo.

Kwanza ni onyo kuwa uepuke kula kumbikumbi wengi wakiwa wabichi kutokana na kuwa wanaweza kukufanya uendeshe.

Ukitaka kufahamu utamu wa mchwa hawa wanaoota mbawa unashauriwa kuwakaanga. Maandalizi ya kumbikumbi huanza na kuwaokota kwenye ardhi baada ya wao kutoka katika vichuguu.

Baada ya kuwaokota, waoshe vyema na maji safi kuondoa vumbi/matope wanayokuwa nayo kwa sababu wengi hupatikana msimu wa mvua.

Bila ya kutumia mafuta kwa sababu wana mafuta mengi, wanawekwa kikaangoni ama kwenye sufuria na kuongezwa chumvi, na kwa kutumia moto usio mkali, wanageuzwa kama njugu hadi wakauke.

Kumbikumbi kisha wanawekwa kwenye chombo bapa kama trei ama mabati na kuanikwa kwenye jua. Tumia mikono yako kuwagusa ili kuhakikisha wamekauka vyema.

Toa mbawa zao kwa kutumia mikono yako. Unaweza pia kutumia uteo ama trei kuwapepeta ili kuondoa mbawa zao. Mara nyingi shughuli ya kupepeta hufanywa nje ya nyumba wakati kuna upepo, ingawa unaweza kutoa mbawa kwa kutoa upepo kwa nguvu kupitia kinywa chako.

Ukimaliza shughuli ya kutoa mbawa, unaweza kutafuta kumbikumbi kama njugu. Baadhi ya wenyeji wa sehemu hii wanasema pia utafurahia kuwateremsha kwa chai isiyo na maziwa. Hata hivyo, walaji wengi wa kumbikumbi huwala kwa ugali.

Vilevile, unaweza kuunda kitoweo kutokana na kumbikumbi yaani ukawakaanga tena kwa kuongeza viungo vingine kama nyanya na kitunguu na hata maziwa ili kuwafanya wawe na supu na watamu zaidi.

Mchuzi wa kumbikumbi huwa tayari baada ya kuchemshwa kwa dakika tano hivi. Wakiwa tayari, wale kwa ugali.

Japo kuna aina 43 ya kumbikumbi wanaoliwa na binadamu ama kupewa wanyama wanaofugwa nyumbani, jamii ya Waluhya hasa wale kutoka kaunti ya Kakamega inatambua na kula aina tano pekee.

Kuna kumbikumbi wakubwa na wanono, ambao wanapendwa sana. Wanaitwa Amafuetere. Aina hii ya kumbikumbi hutoka kwenye vichuguu saa nane usiku mwezi wa Aprili.

Wakazi wengi huwasubiri sana usiku. Wanatumia mitego maalumu kuwanasa. Pia katika zoezi la ‘kuwavuna’, wenyeji wanatumia taa za mafuta ama gesi na kuwaundia nyumba fulani juu ya kichuguu kwa kutumia matawi ya miti inayoweza kujipinda na kuifunika kwa blanketi, shuka ama majani ya ndizi na kuacha mlango mdogo.

Mbele ya mlango huo kuna shimo ndogo ambalo kumbikumbi hutumbukia na kuzolewa. Shughuli ya wakazi kutoka nje usiku wa manane kusubiri mlo huu hata hivyo zimepungua sana baada ya stima kurahisisha mambo.

Walaji wengi wa kumbikumbi sasa huwasha taa za nje ya nyumba zao na kuweka sufuria, karai, ndoo ama beseni kubwa chini ya taa hizo.

Kumbikumbi wanavutiwa na mwangaza huo na kutumbukia humo. Watu wengi pia hurauka mapema asubuhi na utawapata barabarani wakiokota kumbikumbi.

Shughuli ya kutega aina hii ya kumbikumbi pia zimepunguzwa na hatari ya kuvamiwa na nyoka ama wanyama wengine wa mwituni wanaokula kumbikumbi. Hali ya usalama pia si nzuri kwa hivyo watu huhofia kushambuliwa.

Amafuetere ndio kumbikumbi walio na bei ya juu. Kikombe kimoja cha kumbikumbi hawa huuzwa Sh100.

Aina zingine za kumbikumbi zinazofanywa mlo na Waluhya ni Amakabuli wanaopatikana wakati wowote kuanzia saa kumi na mbili jioni wakati wa msimu wa mvua nao Eshirunda wanapatikana mwezi Juni wakitoka kwenye vichuguu kati ya saa kumi na saa kumi na mbili jioni.

Kumbikumbi wa aina ya Tsisisi hupatikana mwezi Agosti/Septemba. Kumbikumbi hawa pamoja na Eshirunda na Amakabuli huwa ni weupe tofauti na Amafuetere ambao ni weusi.

Amakushe nao ni kumbikumbi weusi ambao hupatikana baada ya kulazimishwa na binadamu kutoka katika makao yao kwa nyimbo vichuguu vyao vinapopigwapigwa kwa vijiti fulani. Kikombe kimoja cha Tsisisi, Amakushe, Eshirunda na Amakabuli ni Sh50.

Tahadhari nyingine ni kwamba si kumbikumbi wote huliwa. Inadhaniwa, japo hakuna utafiti wa kuthibitisha, kwamba kumbikumbi wadogo ambao kwa Kiluhya wanafahamika kama Tsimbolombolwe husababishia mlaji matatizo ya masikio.

Humfanya apoteze uwezo wa kusikia. Utafiti unasema kwamba kumbikumbi wana protini nyingi kama tu nyama, ute wa yai au samaki.

Pia, wana mafuta ndio sababu hawapikwi kwa kutumia mafuta. Walaji wengi wa kumbikumbi wanapatikana katika mataifa yanayokuwa, ingawa miaka ya hivi karibuni ulaji wao unasemekana umeanza kupata umaarufu katika mataifa yaliyoendelea.

Kumbikumbi wanaliwa barani Afrika, Asia na Amerika ya Kaskazini na Kusini.