Makala

Aina za pua na maana kwa mujibu wa watafiti

July 2nd, 2019 3 min read

Na MWANGI MUIRURI

WANASEMA kata pua uunge wajihi.

Kamusi ya Kiswahili Sanifu inasema pua ni neno ambalo liko katika ngeli ya I-ZI.

Ukiwa mtaani au kwako nyumbani…popote pale na ushtukie kuna wale wameanza kutilia maanani umbo la pua, usiingiwe na taharuki kwa kuwa labda umewekwa katika darubini ya watafiti wa mtandao wa brainberries.com .

Hao ni wale ambao wametoa matokeo ya utafiti wao unaoonekana kuwa na ucheshi mwingi kuhusu misukumo ya kimaisha inayodadisiwa na umbo la pua.

“Kuna ushahidi kuwa umbo la pua husema mengi kuhusu tabia zako za kimaisha. Pua ni ushahidi mmoja wa urembo au uvutio wa uso wako na katika uso ndio mengi ya kimaisha kukuhusu hujiangazia,” inasema sehemu ya ripoti ya watafiti hawa.

Wanasema kuwa kwa kuangalia tu pua, kuna watafiti wa Kisayansi watakamwambia mtu ikiwa ama ni wa kufanikiwa kimaisha, mtu wa kufikiria na kuwa mweledi wa kutatua masuala nyeti au yeye ni zumbukuku.

Wale ambao wako na pua ambazo matundu yake yameinuka kiasi husemwa kuwa huwa na uwezo wa kunusa hatari ikiwa mbali na ili uelewe kati ya polisi ambao wako kazini kama kipawa au wale walio katika ajira hiyo kama wa kusindikiza tu wenzao, angalia pua zao.

Ukiona yale zimeinuka kidogo kiasi kwamba matundu yake yanakaa kama kamera za darubini, hao ni polisi; ten wa kuzaliwa hasa.

Watafiti hao wanasema kuwa kuna wengine ambao wako na pua ambazo zinakaa kama mwewe.

Pua ambazo zinakaa kama zinakuelekeza sio kidole kwa kuwa pua haina kidole, bali inakuelekeza pua ya lawama.

“Hizo ni pua ambazo huhusishwa sana na wachawi! Aliyekuambia kuwa pua ya aina hiyo inavutia ni mwongo! Ni mojawapo ya pua mbaya zaidi unaweza kuwa nazo katika jamii… Lakini walio na hizo pua, ni viongozi katika fani mbalimbali. Angalia ushahidi miongoni mwa Wazungu sanasana, hasa Kocha Arsene Wenger aliyekuwa mkufunzi wa klabu ya Arsenal nchini Uingereza au chale Mr Bean,” yafichuliwa na ripoti hii.

Kuna pua zingine ambazo zinasemwa kuwa huwa zimeumbwa zikielekeza kona zake juu kama nyota.

Sio lazima iwe ni kuelekeza hizo kona juu kwa njia mbovu, lakini pua hizo huwa na taswira ya kujeruhiwa kupitia kuvurutwa juu!

Ni kama pua aina hiyo huwa imevunjwa katika lile daraja (bridge) la pua ambalo huwa ni katikati mwa pua ambapo ukitembeza kidole juu yake kwenda juu; na hizi ndizo pua ambazo ziko kwa wingi dunia hii na ambazo huhusishwa na watu wa kawaida maishani.

Pua zilizonenepa?

Kuna wengine ambao huwa na pua ambazo zimenona au kunenepa.

Pua za aina hiyo ukizishika, unapata taswira ya kushikashika mandazi yaliyojaa unga ndani.

Pua aina hiyo huonyesha kuwa haikuogopi wewe unayeitazama kwa kuwa imejaza misuli…

“Wale ambao wana pua aina hii hawaogopi lolote… Hawatishwi na masuala ya kimaisha na katika mijadala, watakinga kauli zao kutokana na uvamizi wa kuzidunisha na watazikinga kwa dhati,” wasema wataalamu hao wa pua na umbo.

Kuna umbo lingine la pua kwa jina “Nixon.”

Ni pua ambayo ukiitafutia jina au ufafanuzi utakosa kwa kuwa ni ya kipekee na inaishia kupewa jina la aliye nayo.

Mtukutu

Pua aina hii inasemwa kuwa mwenyewe huwa ni mtukutu na ambaye atakuhadaa kwa kila hila na njama lengo likiwa ni kujinufaisha mwenyewe.

Katika hali hii, ni vyema Wakenya watilie maanani maumbile ya pua za wanasiasa wao hasa wale walio na sakata za kiufisadi.

Kuna wengine ambao wanasemwa kuwa na pua “Roman”.

Ni pua ambayo juu yake inajiangazia kwa kunona katika umbo mfano wa matuta. Ni matuta ambayo husononesha wamiliki wa pua hili kiasi kwamba wengi husaka huduma za kimatibabu kurekebisha umbo hilo.

Lakini walio na pua sampuli hizo wanasemwa kuwa hudumisha urafiki wa dhati na husifika kuwa wazazi bora zaidi.

Haijulikani kama ukipata mwizi amehukumiwa unafaa uangalie umbo la pua za wazazi wake, au mtoto akiwa mtukutu shuleni kabla ya kumwadhibu uwaite wazazi wake na uwaangalie pua ndipo uelewe kama ni wao wa kulaumiwa kutokana na tabia mbovu za hao watoto.

Kunao wengine wanaosemwa au wameorodheshwa kuwa na pua aina ya “Nubian.”

Hili ni pua ambalo linaonekana kama kulikuwa na jaribuio ya kuliponda na hivyo kuliacha likiwa kama linataka kulalia uso na katika harakati hizo, kujipa upana wa kipekee. Ni mapua yanaomilikiwa na, utafiti huo wataja, ‘Waafrika’ kama Beyoncé, Jay Z, Kanye West na Barack Obama.

“Walio na mapua sampuli hii huwa ni wa kuvutia, wako na matarajio makuu ya kimaisha na hufanikiwa sana kimaisha,” wasema.

Pua la Kigiriki ndilo linasemwa kuwa la kuvutia zaidi na halitishi, halikupi wasiwasi wowote na halijiangazii kama lililoumbwa kwa haraka hivyo basi kuwa na mpangilio wa kiholela…

Ni pua ambalo urefu uko sawa, unono uko sawa, upana uko sawa, matundu yake yako sawa na huhusishwa na watu walio na busara na ambao katika utatuzi wao wa masuala ya kimaisha huwa ni kupitia ushirikishi na ubunifu.

Ukisoma haya, kwa kawaida utajipata ukitilia maanani maumbile ya pua za wenyewe na sio ajabu ujipate ukiwacheka wengine au ukisambaza utaalamu huu ambao ni wa kipekee kuhusu kuwachambua watu kupitia umbo la pua yao; na hiyo pia ni raha ya maisha.