Kimataifa

Airtel yalemewa na biashara Afrika, yapanga kung'atuka

May 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya mawasiliano ya simu Bharti Airtel inadaiwa kulenga kuondoka katika Soko la Afrika.

Kampuni hiyo ndiyo mzazi wa Airtel Kenya na katika hatua zake za hivi punde, inalenga kuuza robo ya hisa zake Afrika katika azimio hilo kulingana na ripoti ya vyombo vya habari nchini India.

Ripoti iliyochapishwa katika magazeti India inaonyesha kuwa kampuni hiyo inalenga kupata Sh150 bilioni kwa kuuza sehemu ya hisa zake kwa lengo la kuokoa deni la Sh460 bilioni katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Shughuli ya mauzo hayo inatarajiwa kuzinduliwa Afrika Kusini au Uingereza kulingana na habari hizo.

Mwishoni mwa mwaka jana, Bharti Airtel ilisema ilikuwa tayari kuuza asilimia 20 ya hisa zake ndani ya Airtel Kenya kwa wawekezaji wake humu nchini kabla ya kuondoka nchini kabisa.

Kampuni hiyo inalenga kukomesha biashara zake Kenya, Rwanda na Tanzania na kwa sasa inatafuta mkataba wa kuuza hisa zake kwa kampuni za humu nchini, kununuliwa au kuungana na kampuni zingine.