Habari MsetoSiasa

AISHA JUMWA: Tamaduni mbovu za Mijikenda ndicho kiini cha mimba shuleni

November 13th, 2018 2 min read

Na CHARLES LWANGA

MBUNGE wa Malindi, Bi Aisha Jumwa amesema mila na tamaduni mbovu za jamii ya Mijikenda pamoja na malezi mabovu ndicho chanzo kikuu cha ongezeko la mimba za mapema katika Kaunti ya Kilifi.

Pia, aliwalaumu maafisa wa polisi kwa ongezeko la visa hivyo kwa kutoa leseni za kuruhusu densi za usiku matangani ijulikanayo kama ‘disko matanga’ licha ya serikali kupiga marufuku densi hizo.

Akizungumza alipokuwa akitoa hema na viti kwa viongozi wa dini eneo la Takaye, Bi Jumwa pia aliwaonya akina mama wanaovaa nguo kiholelaholela sawia na wanaoenda baharini kuogelea akisema kuwa imeongeza uzorotaji wa tabia kati ya vijana.

“Kuna baadhi ya wanawake ambao hawaendi kanisani lakini kila Ijumaa wanavaa ‘madera’ ya bei ghali kusindikiza mili na kuhudhuria matanga,” alisema na kuongeza “haya yanajiri wakati wana wao wasichana hawana sodo na baadaye kuanguka kwa mtego wa wanabodaboda ambao huwapa Sh50 na kuwatia mimba.”

Bi Jumwa alizungumza haya kutokana na ripoti ya idara ya watoto Kaunti ya Kilifi iliyoonyesha kuwa takriban wasichana 13,000 kati ya umri 15 na 17 walipata mimba kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Vilevile, aliwataka akina mama wanaoenda kanisani wawe mfano mwema kwa watoto wao wasichana.

“Watoto wako huangalia jinsi unavyovaa na ikiwa unavaa nguo za kubana na kwenda kanisani mtoto wako ataiga mfano huo na ni jambo la aibu sana,” alisema na kuongeza baadhi ya akina mama huvalia vibaya wakienda makanisani ni kama dunia inakuja kuisha leo.”

Bi Jumwa alitaka washikadau wa kiserikali na wale wasio wa kiserikali wafanye mkutano wa dharura ili kupata suluhisho la janga la mimba za mapema.

Pia, alisema watu wengine wameasi mila na utamaduni wao na kufuata mila za kizungu wanazowalelea wana wao.

“Wasichana wanafaa wajue kuwa kupata mimba ni dakika kumi tu au hata nusu dakika na ni jambo la kushangaza kuwa baadhi ya wazazi bado wanawacha wasichana wao watembee zaidi ya dakika 30,”alisema.

wenyewe wakienda shuleni na inafaa tupunguze huo muda,” alisema.

Wakati huo huo, alitoa wito kwa wasichana waliopata mimba kati ya umri 15 na 17 wajitokeze kwa mkutano ofisini mwake ili wajadili na kutafuta suluhisho ya janga la mimba za mapema eneo hilo.