Habari Mseto

Ajabu jamaa kuvalia mavazi ya kike ili kumwibia mteja simu klabuni

February 25th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

POLISI mjini Kisii wanamzuilia mwanamme mmoja aliyejifanya mwanamke kwa kuvalia mavazi ya kike ili kumwibia simu mteja aliyefika kwenye chumba cha burudani kilichoko Nyamataro, viungani mwa mji wa Kisii.

Kisa hicho cha kushangaza, kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Nyakoe na jamaa wawili ambao ni wasimamizi wa klabu kiitwacho BMW, kwamba mmoja wa wateja wao alikuwa amelalamikia kuibiwa simu yake na mhudumu wa baa hiyo.

Baada ya kugundua kwamba simu yake ilikuwa imeibiwa, mteja huyo alikwenda kwa wasimamizi hao na kuwaarifu kilichokuwa kimetokea.

Wasimamizi hao walimuita mhudumu huyo mshukiwa kumchunguza lakini aliaanza kujikanganya.

Baada ya kuona maswali yanamlemea, mwanaume huyo aliyejifanya mwanamke aligeukia mguu niponye.

Lakini umati uliokuwa nje ya klabu hicho ulimwandama na kumkamata kabla hajaenda mbali na simu iliyokuwa imepotea ikapatikana.

Raia hao walipomwangalia vizuri, waligundua kuwa jamaa huyo alikuwa mwanamume aliyevalia tu mavazi ya kike ili kuwapumbaza waja wengine.

Katika video ya dakika nne na sekunde 41 ambayo iliambatanishwa na ripoti ya polisi, ambayo Taifa Leo Dijitali ilifanikiwa kuiona, maafisa waliomkamata wanaonekana wakimvua nguo zote jamaa huyo ili kudhibitisha jinsia yake.

Huku polisi hao wakimdhihaki jamaa huyo kwa kitendo hicho, maafisa hao wanasikika wakimuuliza ni kwa muda upi ambapo amehudumu klabuni humo akiwa amejifanya mwanamke.

“Unasema unaitwa Felister? Umefanya kazi hii kwa muda gani?” Afisa mmoja anauliza huku jamaa huyo akimjibu kuwa amefanya kazi BMW kwa miezi miwili.

Haikubainika mara moja jinsi jamaa huyo amekuwa akijifanya mwanamke bila wenzake kufahamu kwa muda huo wote lakini uchunguzi kwa tukio hilo umeanzishwa.

Mojawapo ya mavazi aliyovalia jamaa huyo ni sidiria.

Ndani ya sidiria hiyo, alikuwa ameweka vipande vya nguo kuukuu ili kughushi kuwa alikuwa na maziwa kama yale ya wanawake.

[email protected]